NA MWANDISHI WETU
Katika tukio adimu, lenye uzito wa kitaifa na la kihistoria, Jamii ya Kimaasai nchini Tanzania imeonyesha heshima ya hali ya juu kwa Katiba na Demokrasia kwa kuahirisha zoezi lao muhimu la kimila la tohara ili kuhakikisha vijana zaidi ya 1,000 wanashiriki kikamilifu katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Uamuzi huu uliotolewa na Laigwanani Mkuu, Isack Ole Kisongo Meijo, si tu tamko la uzalendo, bali ni pigo zito kwa wale wote wanaopanga njama za vurugu, maandamano, au mbinu za kuvuruga amani na mfumo wa kikatiba wakati au baada ya uchaguzi.
Darasa la Uzalendo kwa Taifa
Kwa kuahirisha tukio hilo kuu la kimila, ambalo kwa kawaida huathiri uwezo wa vijana wengi kushiriki kupiga kura, Maasai wameweka kiwango kipya cha kuheshimu mfumo wa kidemokrasia.
Laigwanani Ole Kisongo alisisitiza wazi kuwa amani, uwajibikaji wa kiraia, na kura ni kipaumbele kinachozidi hata matukio makuu ya utamaduni wao.
"Jamii ya Kimaasai imeonesha mfano wa kuigwa. Huu ndio uzalendo tunaoutaka. Kura ndiyo sauti ya maendeleo, na amani ndiyo msingi wa taifa letu," alikariri Mkuu wa Mkoa wa Arusha, CPA Amos Makalla, akipongeza hatua hiyo.
Pigo kwa Wapanga Vurugu
Kitendo hiki cha Maasai kimepokelewa kama ishara ya wazi kwamba Watanzania wanajua wanachotaka: Wanaamini katika mabadiliko ya kimaendeleo yanayofuata Katiba na yanayotawaliwa na amani na utulivu.
Uamuzi wa Waasai kuahirisha mila yao kwa ajili ya kupiga kura unatoa ujumbe mkali na wa moja kwa moja kwa wale wanaopanga mbinu za kuingia madarakani au kuleta mabadiliko kupitia njia za vurugu au maandamano yasiyo halali: Watanzania wamechagua sanduku la kura, siyo vurugu.
Kabla ya sherehe kuu za tohara, Maasai wameweka neno la mwisho: Wanaheshimu mfumo wa kidemokrasia na Katiba.
Ikiwa kabila lenye utamaduni tajiri linaamini kwenye kura, maana yake ni kwamba njia ya amani ndiyo njia pekee ya mabadiliko inayokubalika na Watanzania walio wengi.
Waasai wanawaonyesha Watanzania wote njia: Kura Kwanza, Vurugu Haikubaliki. Hii inathibitisha kuwa utashi wa Taifa ni kuona maendeleo ya nchi yanaendelea katika mazingira ya utulivu na uwajibikaji wa kikatiba.
Post a Comment