" MADEREVA WA MABASI WAHIMIZWA KUKATA STIKA ZA “NENDA KWA USALAMA” KWA NJIA YA MTANDAO

MADEREVA WA MABASI WAHIMIZWA KUKATA STIKA ZA “NENDA KWA USALAMA” KWA NJIA YA MTANDAO

Madereva wa mabasi yaendayo mikoani wamepewa elimu ya jinsi ya kukata stika za Nenda kwa Usalama kwa njia ya mtandao, sambamba na kufanya ukaguzi wa vyombo vyao vya moto kwa wakaguzi wa magari ili kuhakikisha usalama barabarani.

Elimu hiyo imetolewa na Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Wilaya ya Shinyanga, Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Zainabu Mangara, katika Stendi Kuu ya Mabasi ya Mkoa wa Shinyanga, ambapo amewaelekeza madereva namna ya kuingia kwenye mfumo na kufuata taratibu sahihi za kukata stika hizo mtandaoni.

ASP Mangara amesema mfumo huo ni sehemu ya jitihada za Jeshi la Polisi kuhakikisha magari yote yanayofanya safari za mikoani yanakuwa salama kabla ya kuanza safari, sambamba na kurahisisha upatikanaji wa huduma bila foleni au usumbufu.

Aidha, amewataka madereva kuhakikisha magari yao yanapelekwa kwenye vituo vya Polisi vilivyoidhinishwa kwa ajili ya ukaguzi, ili kubaini mapema kama kuna kasoro zozote kwenye vyombo hivyo na kuchukua hatua za matengenezo kabla ya safari.

“Tunawasihi madereva wote kuzingatia matakwa ya Sheria za Usalama Barabarani na kukata stika hizi kwa njia ya mtandao ili kuepuka usumbufu na kuhakikisha usalama wa abiria,” amesema ASP Mangara.

Madereva hao kwa upande wao wamepongeza hatua hiyo, wakisema mfumo wa mtandao utapunguza gharama na muda waliokuwa wakitumia kufuatilia huduma hiyo kwa njia ya kawaida.


Post a Comment

Previous Post Next Post