Walimu wanawake wa Manispaa ya Shinyanga wamehimizwa
kuendeleza umoja, mshikamano na weledi katika kazi zao ili kuimarisha ubora wa
elimu na kukuza maendeleo ya kijamii na kiuchumi kupitia taaluma yao.
Kauli hiyo imetolewa katika kongamano la walimu
wanawake wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Manispaa ya Shinyanga,
lililofanyika Oktoba 24, 2025, likiwa na lengo la kuwajengea uwezo katika
nyanja za uongozi, uchumi, sheria na ustawi wa jamii.
Kongamano hilo limeandaliwa na Kitengo cha Walimu
Wanawake Manispaa ya Shinyanga chini ya uongozi wa Mwenyekiti Mwl. Subira
Mustafa Kuhenga, kwa ushirikiano na Mwenyekiti wa upande wa KE Rose Mabana na Mweka
Hazina Stella Halimoja.
Katika kongamano hilo, mada mbalimbali zimejadiliwa
ikiwemo Sheria ya Ndoa, Mirathi na Talaka, Mahusiano Kazini, Uchumi na
Mikopo yenye masharti nafuu, Ujasiriamali, Uongozi wa Mwanamke na Mapambano
dhidi ya Ukatili wa Kijinsia.
Akizungumza wakati wa kikao hicho, Afisa Utumishi wa
Manispaa ya Shinyanga, Bw. Jackson Mwakisu, amesema mwalimu mwanamke ana nafasi
kubwa katika kulilea jamii na kujenga uchumi wa familia, hivyo ni muhimu
kuwekeza katika mafunzo yatakayowasaidia kuwa viongozi bora, wachapakazi na
wenye dira.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Walimu
Manispaa ya Shinyanga, Mwl. Subira Mustafa Kuhenga, amesema lengo la
makongamano hayo ni kuhakikisha walimu wanawake wanapata elimu ya kujitambua,
kujenga kujiamini na kuimarisha ushirikiano katika kazi na jamii.
Ameongeza kuwa kongamano hilo limekuwa jukwaa la
kuunganisha walimu katika kujadili changamoto zinazowakabili na kuzitafutia
suluhisho la pamoja.
Aidha, Mwanasheria Ruth Ndagu, akiwasilisha mada ya Sheria
ya Ndoa na Mirathi, amesema ni muhimu kwa walimu wanawake kuelewa haki zao
za kisheria ili kuepuka kudhulumiwa katika mali, mirathi au ndoa, na
kuwaelimisha wanafunzi wao juu ya haki na wajibu katika jamii.
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Taasisi ya
Wanawake Laki Moja Mkoani Shinyanga, Bi. Anascolastica Ndagiwe, amewataka
walimu wanawake kutumia utu na weledi wao kupinga ukatili wa kijinsia
mashuleni, akisisitiza kuwa mwalimu ndiye nguzo muhimu ya kumlinda mtoto dhidi
ya manyanyaso na malezi yasiyo bora.
Naye Katibu wa Kitengo cha Walimu Wanawake Taifa, Bi.
Elizabeth Werema, amesema mapambano dhidi ya ukatili hayaanzi shuleni pekee
bali nyumbani, hivyo kila mwalimu anatakiwa kuwa kioo cha maadili, malezi na
heshima kwa jamii.
Mjumbe wa Kamati Tendaji ya CWT Taifa, Bi. Grace Kulwa,
amebainisha kuwa kongamano hilo limekuwa fursa kwa walimu wanawake
kubadilishana uzoefu, kujifunza mbinu za kuimarisha mahusiano kazini, na
kuongeza kipato kupitia miradi ya ujasiriamali na uwekezaji.
Akihitimisha kongamano hilo, Mwenyekiti wa Kitengo cha
Walimu Wanawake Taifa, Bi. Neema Obedi, amesema mafunzo hayo yatasaidia kujenga
kizazi cha walimu wanawake wenye uelewa mpana, wanaoweza kulea kizazi cha
wanafunzi wachapa kazi, wenye nidhamu na uzalendo.
Mwenyekiti wa upande wa KE Rose Mabana, akizungumza.
Mwenyekiti wa upande wa KE Rose Mabana, akisoma risala ya walimu wanawake Manispaa ya Shinyanga.

Post a Comment