" MAELEKEZO KWA WAPIGA KURA YATOLEWA

MAELEKEZO KWA WAPIGA KURA YATOLEWA

Na, Egidia Vedasto, Misalaba Media - Arusha. 

Tume ya taifa ya uchaguzi kupitia kwa msimamizi mkuu wa uchaguzi jimbo la Arusha Mjini Shaban Manyama ametoa tangazo la uchaguzi kwa wananchi wote waliojiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura la Tume huru ya taifa ya uchaguzi kuelekea siku hiyo oktoba 29 mwaka huu. 

Akizungumza na waandishi wa habari jijini humo Manyama amesema kupiga kura ni haki ya kila mtanzania mwenye akili timamu na umri kuanzia miaka 18.

Msimamizi Mkuu wa Uchaguzi Jimbo la Arusha Mjini (katikati) Shaban Manyama_

Aidha amesema kuwa uchaguzi huo wa Rais, Wabunge na Madiwani unatarajiwa kufanyika siku ya jumatano Oktoba 29 mwaka huu. 

"Vituo vilivyotumika kuandikishia wapiga kura ndivyo vitakavyotumika kupigia kura, vituo vyote vitafunguliwa saa moja kamili asubuhi na kufungwa saa kumi kamili jioni (1:00-10:00)", 

" Vituo vya kupigia kura vya Magereza vitafunguliwa saa mbili kamili asubuhi na kufungwa saa tisa kamili   alasiri (2:00-9:00), pamoja na hayo kwa kila kituo cha kupigia kura zimebandikwa taarifa kama mfano wa karatasi ya kura yenye majina na picha za kila mgombea pamoja na nembo za vyama vyao vya siasa kwa uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, "amesema.

Vilevile amefafanua  kuwa taarifa nyingine ni orodha ya majina ya wapiga kura walioandikishwa na Tume huru ya taifa na orodha ya wapiga kura walioruhusiwa kupiga kura moja tu ya Rais. Wananchi wote wameombwa kupitia taarifa hizo ili kutambua mapema vituo watakavyopigia kura na kuona mfano wa karatasi ya kura. 

Hata hivyo wananchi wamekumbushwa kufika kituo cha kupigia kura na kadi ya mpiga kura huku akisema kwa aliyepoteza kadi yake, ataruhusiwa kupiga kura katika kituo alichojiandikishia akiwa na leseni ya udereva, kitambulisho cha Taifa (NIDA) au hati ya kusafiria.


 



Post a Comment

Previous Post Next Post