" MAKALANI 425 WAONGOZAJI WA VITUO VYA KUPIGIA KURA WAAPISHWA NA KUPEWA MAFUNZO

MAKALANI 425 WAONGOZAJI WA VITUO VYA KUPIGIA KURA WAAPISHWA NA KUPEWA MAFUNZO

NA ELIAS GAMAYA - SHINYANGA

Makalani 425 waongoza wa vituo vya kupigia kura katika Jimbo la Shinyanga Mjini wameapishwa na kupewa mafunzo maalum ya usimamizi wa uchaguzi, ambapo wametakiwa kuzingatia viapo vyao ili kuhakikisha zoezi la upigaji kura linakuwa huru, haki na kwa amani katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Jumatano, Oktoba 29, 2025.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Shinyanga Mjini, Mwl. Ally Liuye, amewataka makalani hao kutekeleza wajibu wao kwa uadilifu na kufuata viapo walivyoapa, ikiwemo kiapo cha kujitoa katika chama chochote cha siasa na kiapo cha kutunza siri za uchaguzi.

“Ni wajibu wenu kuhakikisha mnasimamia mchakato huu kwa uaminifu na kutenda haki kwa wagombea wote. Zoezi la uchaguzi ni wajibu wa kikatiba unaohitaji uadilifu, uwazi na uzalendo,” amesema Mwl. Liuye.

Ameeleza kuwa uteuzi wa makalani hao umezingatia masharti ya Kifungu cha 76 cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya mwaka 2024, sambamba na Ibara ya 74(6) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.

Baadhi ya makalani walioshiriki mafunzo hayo, Jackline Msuya na Emmanuel Kasunga, wameahidi kufanya kazi kwa kuzingatia kanuni, taratibu na sheria za uchaguzi, huku wakitoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki uchaguzi huo kama njia ya kuchagua viongozi bora kwa maendeleo ya taifa.

“Kura yako ni sauti yako. Tunawahimiza wananchi wote wa Shinyanga kutumia haki yao ya kikatiba kupiga kura ili kuchagua viongozi wanaostahili,” walisema.

Jimbo la Uchaguzi la Shinyanga Mjini lina jumla ya kata 17 na vituo vya kupigia kura 391, ambapo kaulimbiu ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu ni:“Kura Yako Haki Yako — Jitokeze Kupiga Kura.”



 

 

🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA

Post a Comment

Previous Post Next Post