Madereva wa magari ya mizigo wamepatiwa elimu ya usalama barabarani wakihimizwa kuacha mara moja tabia ya kuwaruhusu matingo wao kuendesha magari hayo hasa nyakati za usiku, jambo ambalo limeelezwa kuwa ni hatari na kinyume cha sheria.
Akitoa elimu hiyo, Askari Polisi wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Shinyanga, Sajenti David Ndimila, amewataka madereva hao kutambua kwamba matingo hawana sifa za udereva, hivyo kuwaruhusu kuendesha magari ni kuhatarisha maisha yao na watumiaji wengine wa barabara.
Amesema vitendo hivyo vimekuwa vikichangia ajali nyingi zisizo za lazima, hasa nyakati za usiku, kutokana na ukosefu wa ujuzi na uelewa wa sheria za barabarani kwa watu hao.
Aidha, Sajenti Ndimila amewahimiza madereva wa magari makubwa ya mizigo kuwa mabalozi wa usalama barabarani kwa kuwaelimisha matingo wao kujiunga na vyuo vya udereva vilivyothibitishwa na serikali ili wapate ujuzi na leseni halali kabla ya kuanza kuendesha magari.

Post a Comment