Na: Dkt. Reubeni Lumbagala, Misalaba Media -Tanga
Kila baada ya miaka mitano nchi yetu inafanya Uchaguzi Mkuu wa kuchagua viongozi katika nafasi za Urais, Ubunge na Udiwani ili kuwatumikia wananchi. Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imeshatangaza Jumatano ya Oktoba 29, 2025 kuwa ndiyo siku ya Uchaguzi Mkuu. Katika siku hii, wananchi wanapata fursa ya kwenda kupiga kura katika vituo walivyojiandikisha ili kutimiza haki yao ya kikatiba ya kuchagua viongozi ambao ni muhimu katika kufanikisha mipango ya maendeleo.
Vituo vya kupigia kura vitafunguliwa kuanzia saa moja kamili asubuhi na kufungwa saa kumi kamili jioni. Katika masaa haya kumi, wananchi waliojiandikisha wanapata fursa ya kipekee ya kuamua hatma ya maisha yao katika kipindi cha miaka mitano ijayo yaani 2025-2030. Kwa kuzingatia ukweli kuwa siasa inaamua hali ya maisha ya wananchi itakavyokuwa, ni muhimu sana kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura kuchagua viongozi ambao wanadhani wanafaa katika kuwatumikia.
Katika Uchaguzi Mkuu huu, INEC inachagiza zoezi hili la Uchaguzi kupitia kaulimbiu isemayo "Kura Yako Haki Yako Jitokeze Kupiga Kura." Ni muhimu Kwa wananchi kuzingatia kuwa kupiga kura ni haki yao tena ni haki yao ya kikatiba na wakati wa kutimiza haki hiyo ni Oktoba 29, kujitokeza kwa wingi kupiga kura.
Wananchi wanahitaji kuongozwa na viongozi wachapakazi, waadilifu na wazalendo ambao kwao uongozi ni utumishi. Njia pekee ya kuwapatia viongozi wa aina hiyo ni kwenda kupiga kura Oktoba 29. Kura moja ya mwananchi atakayoipiga inayo mchango mkubwa wa kuleta mabadiliko chanya ya kimaendeleo katika Kata, Jimbo na Taifa kwa ujumla wake.
Kwa kuwa siku ya kupiga kura imeshatangaza sana na wananchi wengi wanafahamu siku hiyo, ni muhimu sasa kwa kila mwananchi kuweka ratiba zake vizuri ili ifikapo Oktoba 29, jambo liwe ni kupiga kura na kuendelea na shughuli nyingine za kimaisha. Kiserikali, siku hii itakuwa ni siku ya mapumziko kitaifa ili kutoa fursa kwa wananchi kushiriki kikamilifu kupiga kura bila kikwazo.
Siku zinazidi kuyoyoma kufikia Oktoba 29 ambayo ni siku ya maamuzi muhimu kwa mustakabali wa maendeleo na Taifa letu. Itapendeza kila mwananchi aliyejiandikisha kutimiza haki yake kwa kwenda kupiga kura ili kuchagua viongozi wanaofaa kuongoza kwa maendeleo endelevu. Kutokupiga kura ni kujidhulumu nafsi, ni kuwapa wengine mamlaka ya kukuchagulia kiongozi, ni kutothamini hatma ya miaka mitano ijayo, jambo ambalo ni baya sana.
Ewe mwananchi mwenzangu, usipange kukosa kupiga kura Oktoba 29, kumbuka kuwa fursa hii hujitokeza mara moja katika kipindi cha miaka mitano. Uchaguzi Mkuu ni fursa ya kipekee ya kuamua hatma ya maisha yetu na ya watoto wetu, ni nafasi ya kuichangamkia na si kuichezea wala kuipuuzia. Oktoba 29, toka nyumbani kwako kapige kura kwa mustakabali wa maendeleo kwani kwa kuwapatia viongozi bora ni mwelekeo mzuri wa kufikia maendeleo yenye tija.
Post a Comment