" RC MHITA AKABIDHI MAGARI 5 MAPYA KWA JESHI LA ZIMAMOTO SHINYANGA, ASEMA YATASAIDIA KUOKOA MAISHA ZAIDI

RC MHITA AKABIDHI MAGARI 5 MAPYA KWA JESHI LA ZIMAMOTO SHINYANGA, ASEMA YATASAIDIA KUOKOA MAISHA ZAIDI

 

Na Johnson James, Shinyanga

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, kwa niaba ya wananchi wa mkoa huo, amezindua na kukabidhi rasmi magari matano mapya kwa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali katika kuboresha huduma za dharura na uokoaji mkoani humo.

Zoezi hilo limefanyika katika viwanja vya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, ambapo RC Mhita aliwataka maafisa wa Zimamoto kuyatunza magari hayo na kuyatumia kwa ufanisi mkubwa, huku akiwaasa wananchi kuyatumia kwa wakati sahihi pale kunapotokea majanga kama moto au ajali.

"Magari haya ni kwa ajili ya kuokoa maisha. Tunahitaji ushirikiano kati ya jamii na Jeshi la Zimamoto. Wananchi watumie huduma hizi kwa wakati, na Jeshi lihakikishe magari haya yanatunzwa vizuri kwa manufaa ya wote," alisema Mhita.

Kwa upande wake, Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Shinyanga, Thomas Majuto, amesema ujio wa magari hayo ni ukombozi mkubwa kwao kwani awali walikuwa na magari mawili pekee, lakini sasa wamefikia matano, hali itakayoongeza ufanisi kwenye shughuli za uokoaji.


Magari yaliyokabidhiwa ni pamoja na:  

- Gari kubwa la kuzimia moto

Magari mawili ya kubebea wagonjwa  

- Gari dogo la mitambo ya mawasiliano  

- Gari la ukaguzi

Majuto amesema ujio wa magari hayo pia unapanua uwezo wa kufika maeneo mengi kwa haraka na kutoa huduma za kisasa, na hivyo kusaidia kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza wakati wa majanga.

RC Mhita amesisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kuboresha huduma za uokoaji nchini, ili kuhakikisha maisha na mali za wananchi zinalindwa ipasavyo.


Post a Comment

Previous Post Next Post