Na Mwandishi wetu
Tanzania imeweka historia thabiti katika utekelezaji wa miradi ya maji. Uhalisia huu unamwita kila Mtanzania kuona picha kubwa ya maendeleo badala ya kuruhusu matukio ya kipepee (isolated incidents) kuathiri mtazamo wetu.
Malalamiko madogomadogo kuhusu maji yasiyokidhi au haja ya kufuata maji mbali bado yanaweza kutokea, lakini kasi ya utekelezaji na ukubwa wa miradi inathibitisha kuwa kelele hizo ni suala la muda tu zitaisha. Kazi imefanywa kubwa, na inaendelea kufanywa kwa kasi ya ajabu.
Mafanikio haya yanathibitisha dhamira ya dhati ya Serikali kuhakikisha kila Mtanzania, hasa mama na dada zetu, wanapata maji safi na salama karibu na makazi yao.
Tangu Novemba 2020 hadi Novemba 2024, Serikali kupitia wizara husika imetekeleza miradi 1,633 ya maji, ambapo 1,335 ni ya vijijini na 298 ya mijini.
Utekelezaji huu wa nguvu uliofanywa kwa wakati mmoja, umewezesha upatikanaji wa Maji Vijijini kuongezeka kutoka asilimia 70.1 hadi 79.6. Aidha upatikanaji wa maji mijini umeongezeka kutoka asilimia 84 hadi 90.
Hii ina maana kuwa mamilioni ya Watanzania sasa wana unafuu, na Serikali imeweka misingi thabiti ya maendeleo endelevu katika sekta ya maji.
Uwekezaji wa kimkakati unaonyesha jinsi matatizo yanavyotatuliwa kwa mizizi, siyo kwa matawi:Arusha: Mradi mkubwa wa kihistoria umeongeza uzalishaji wa maji kutoka lita milioni 40 hadi milioni 200 kwa siku, na kuboresha huduma kutoka saa 12 hadi saa 24 kwa siku.
Serikali pia imefufua miradi iliyokwama kwa miongo kadhaa, ikiwemo mradi wa Same–Mwanga–Korogwe unaonufaisha zaidi ya wananchi 400,000, pamoja na kukamilisha miradi 157 mingine ya maji vijijini.
Pia serikali imekamilisha mabwawa 12 ya maji likiwemo bwawa la Muko, lililoongeza huduma ya maji kwa wananchi 450,000 wa Mwanza.
Kupitia Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano Dhidi ya UVIKO-19, miradi 218 imekamilika na kunufaisha zaidi ya wananchi milioni 2.09 nchini.
Kwa sasa, Serikali inaendelea na ujenzi wa bwawa la Kidunda mkoani Morogoro, ambalo litahakikisha upatikanaji wa maji ya uhakika katika Jiji la Dar es Salaam. Miradi mingine mikubwa ni ya Ziwa Victoria kuelekea Tinde na Shelui, na ile inayoendelea Kigoma, Misenyi, na Simanjiro, inathibitisha dhamira ya nchi kufikia asilimia 100 ya upatikanaji wa maji.
Kuelekea Uchaguzi: Chagua Maono ya Maendeleo
Mafanikio haya yanathibitisha kuwa upatikanaji wa maji safi na salama ni haki ya kila Mtanzania. Kuelekea uchaguzi, ni muhimu kwa wananchi kutambua: matukio ya kipekee ya changamoto za maji yaliyobaki hayapaswi kufunika maendeleo makubwa yaliyofanywa kwa maono na mipango ya kitaifa.
Tunahitaji kuendeleza kasi hii. Miradi mikubwa imeshafika mbali sana, na sasa tunahitaji kuchagua viongozi wenye maono ya kuitunza, kuisimamia na kuimaliza kabisa safari hii ya maji, ili kuhakikisha kwamba kelele za kufuata maji historia. Huu ndiyo mfano halisi wa uongozi unaoweka utu na uhai wa mwananchi mbele.
Post a Comment