"
VIKUNDI VYA VIJANA VYASHUKURU SERIKALI YA AWAMU YA SITA KWA MIKOPO YA HALMASHAURI
Na Osama Mohamedi chobo, Misalaba Media - kilwaVikundi vitatu vya vijana katika Kata ya Chumo, Jimbo la Kilwa Kaskazini, vimeishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwawezesha kiuchumi kupitia mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri.Vijana hao walitoa pongezi hizo wakati wa mkutano wa kampeni za ubunge uliofanyika katika kata hiyo, wakibainisha kuwa wamepata pikipiki (bodaboda) 13 zilizotolewa na Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa, hatua ambayo imekuwa chachu ya mabadiliko katika maisha yao ya kila siku.Wakizungumza kwa niaba ya wenzao, vijana hao walisema mikopo hiyo imewasaidia kuongeza kipato, kujiajiri, na kupunguza utegemezi, hivyo kuwa kichocheo cha maendeleo ya vijana katika eneo hilo. Wameahidi kuendelea kuiunga mkono Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kutambua jitihada zake katika kuwainua wananchi wa hali zote.Kwa upande wake, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Mkoa wa Lindi, Patrick Mangarinja, aliwahakikishia vijana hao kuwa chama na serikali bado vinaendelea kuthamini mchango wa vijana katika ujenzi wa Taifa. Alisema kuwa ilani ya CCM imeweka mkakati madhubuti wa kuhakikisha mikopo ya halmashauri inaendelea kuwafikia walengwa kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kujitegemea kiuchumi.Naye mgombea ubunge wa Jimbo la Kilwa Kaskazini, Mhe. Kinjikitile Ngombale Mwiru, aliwataka vijana hao kuendeleza imani yao kwa CCM, akisisitiza kuwa chama hicho kimeendelea kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha wananchi wote wanapata fursa za kiuchumi.Mhe. Ngombale Mwiru aliongeza kuwa yupo tayari kushirikiana na makundi yote ya kijamii kuhakikisha wananchi wanazitambua na kuzitumia fursa zilizopo nchini kwa maendeleo yao binafsi na ya Taifa kwa ujumla.
Mgombea ubunge wa Jimbo la Kilwa Kaskazini, Mhe. Kinjikitile Ngombale Mwiru.




Post a Comment