" WAMILIKI WA GEREJI BUBU ARUSHA KUKIONA CHA MOTO.

WAMILIKI WA GEREJI BUBU ARUSHA KUKIONA CHA MOTO.

Na Egidia Vedasto - Misalaba Media, Arusha. 

Wamiliki wa gereji bubu Jijini Arusha wameagizwa kujisalimisha maramoja katika mamlaka husika ili kubainika usajili wao kwa lengo la kuungana na wenzao katika maeneo yaliyopangwa. 

Mkuu wa wilaya Arusha Joseph Mkude mesema hayo katika mkutano wa hadhara wa kusikiliza kero za mafundi gereji katika eneo la Suye, ambapo amewahakikishia kumaliza kero zao zinazowakabili ikiwemo kutishiwa kunyanganywa eneo lao na halmashauri ya jiji hilo. 


"Mimi sio mtu wa maneno tu bali vitendo, nitahakikisha mnapata hati miliki ya umoja wenu na si mtu mmoja mmoja ili fani hii iwe muendelezo wa  manufaa ya kizazi hiki na kizazi kijacho"

"Nitahakikisha mnapatiwa Mtaalam wa kuwasaidia nna ya kupata mikopo ili muwe miongoni mwa wanufaika wa mikopo ya halmashauri. Matamanio yangu ni kuona nanyi mnainua kipato chenu taifa kwa ujumla" amesema. 

Hata hivyo Mkude ametoa onyo kali kwa waendesha bodaboda ambao bado hawajaondoa viripuzi katika pikipiki zao. Amesema atakayebainika faini ya shilingi milioni moja itamhusu. 

Katibu wa mafundi gereji  wa Krokoni Godfrey Majangu akisoma risala yake mbele ya Mkuu wa Wilaya amesema wanaamini ziara hiyo itakuwa mwarobaini kw changamoto zilizowakabili kwa kipindi kirefu. 

Ameomba wawezeshwe kupata mikopo, kupata hati ya umiliki, kuboreshwa kwa miundombinu yao, amesema malengo yao makuu ni kuongeza wananfunzi ili kukabili ukosefu wa ajira unaowakumba vijana wengi nchini. 

Mgombea udiwani kata ya Kimandolu Abraham Mollel ameiomba TARULA NA TANROADS kufanyia kazi kwa haraka suala la makorongo ili kuwaondolea adha wananchi wa maeneo hayo.


"Kipekee nawashukuru sana Mafundi wetu wa hili eneo, mmekuwa mkisaidia kuwavusha watoto wetu kwenda shule kipindi cha mvua maji yanapojaa, mtaa wetu huu una huduma muhimu za kijamii ikiwemo shule ya msingi na sekondari, kanisa lakini pia wafanyabiashara wanaoingizia taifa mapato. Naomba suala hili liangaliwe kwa jicho la pekee" amesema. 

Mmoja wa mafundi hao Ibrahim Mkuruzi amesema ana imani na serikali ya awamu ya sita na anamshukuru Daktari Samia Suluhu Hassan kuwateua viongozi makini katika Jiji la Arusha. 

"Nina imani nawe katika kuhakikisha unatuletea maendeleo, naomba maombi yetu yazingatiwe ili tufanye kazi yetu kwa amani. Tulikuja vijana na sasa tumekuwa wazee na tunao wazee wenye mika zaifi ya sabini hapa, mtukumbuke maana tuna imani kubwa nanyi viongozi wetu" amesema. 

Mkude ametumia nafasi hiyo kuwasihi wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura tarehe 29 Oktoba mwaka huu ili kuchagua viongozi bora watakaoleta maendeleo ya nchi.

Post a Comment

Previous Post Next Post