DKT. MARGARETH NDONDE ASIMIKWA KUWA MCHUNGAJI SHEMASI DAYOSISI YA SHINYANGA.
Officialgamaya0
Askofu wa Dayosisi ya Shinyanga, Mhashamu Johnson Japheth
Chinyong'ole, amemsimika Dkt. Margareth Aidan Ndonde katika daraja takatifu la
ushemasi, katika ibada maalumu iliyofanyika katika Kanisa la Anglikana
Mtakatifu Andrew Kitangili, Dayosisi ya Shinyanga.
Dkt. Margareth, ambaye pia ni Katibu wa UMaki na mratibu wa
shughuli za maendeleo ya wanawake na watoto ngazi ya taifa, amepokea daraja
hilo kama hatua muhimu ya kulitumikia Kanisa na jamii kupitia wito wake wa
kichungaji.
Akizungumza wakati wa ibada hiyo, Askofu Chinyong'ole amesisitiza
umuhimu wa wachungaji kutanguliza unyenyekevu, utii na upendo katika utumishi
wao huku akibainisha kuwa kazi ya kichungaji ni dhamana ya kiroho yenye uzito
mkubwa kwa waamini na jamii kwa ujumla.
“Huduma ya kichungaji si cheo, bali ni mwito wa kujitoa,
kubeba mizigo ya wengine na kuwa mfano wa imani. Mungu awasaidie muwe taa na
chumvi ya dunia,” amesema Askofu Chinyong'ole.
Kwa upande wake Dkt. Margareth amehidi kulitumikia Kanisa
kwa bidii, uadilifu na moyo wa kujitolea ili kuendeleza gurudumu la injili na
kuinua huduma za Kanisa kwa wanawake, watoto na jamii kwa ujumla.
“Ninaipokea dhamana hii kwa moyo wa shukrani na
unyenyekevu. Nitafanya kazi kwa ushirikiano, upendo na uaminifu ili nione
injili ikisonga mbele,” amesema Shemasi Dkt. Margareth.
Naye Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Mtakatifu Andrew
Kitangili, Joan Ndabakubije, amempongeza Askofu Chinyong'ole kwa kuendelea
kuwaamini wachungaji wanawake, huku akisema kitendo hicho kinaimarisha imani na
kuhamasisha wanawake wengi zaidi kujitoa katika huduma za uinjilisti.
“Tunaishukuru Dayosisi kwa kutuamini kama wanawake.
Tutaendelea kufanya kazi kwa bidii na uaminifu ili kustahili imani hii na
kuthibitisha kuwa wanawake pia wanaweza kulitumikia Kanisa kwa ufanisi na
ushupavu,” amesema Mch. Ndabakubije.
Post a Comment