" SERIKALI YAKEMEA VITENDO VYA KUCHOCHEA TAHARUKI KWA KUCHAPISHA PICHA ZA KUTIA HASIRA

SERIKALI YAKEMEA VITENDO VYA KUCHOCHEA TAHARUKI KWA KUCHAPISHA PICHA ZA KUTIA HASIRA

Serikali, kupitia Wizara ya Afya na Msemaji Mkuu wa Serikali, imelaani na kukemea vikali kitendo cha baadhi ya watu kutengeneza na kusambaza picha na video za uongo zenye nia ya kuchochea taharuki na hasira miongoni mwa Watanzania.

Kukemea huku kunafuatia kuonekana kwa picha na video zinazoonyesha miili ya watu imewekwa pamoja, ambapo watengenezaji wa picha hizo walidai kuwa tukio hilo limetokea katika Hospitali ya Mwananyamala jijini Dar es Salaam.

Katika taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini cha Wizara ya Afya leo, Wizara ilikanusha vikali uhalisi wa picha hiyo, ikifafanua kuwa video hiyo imetengenezwa na wahalifu wenye nia ya kuichafua nchi.

“Wizara ya Afya imeona picha ya video inayoonyesha miili ya watu ikiwa imewekwa pamoja na kueleza kwamba hapo ni Hospitali ya Mwananyamala, Dar es Salaam. Wizara inapenda kukanusha uhalisi wa video hiyo ambayo imetengenezwa na wahalifu wenye nia ya kuichafua nchi yetu,” ilisomeka sehemu ya taarifa hiyo.

Wizara imewataka wananchi kuacha mara moja kusambaza picha hizo kwa kuwa kufanya hivyo ni kuvunja Sheria, na imewataka Watanzania kuendelea kuziamini huduma zinazotolewa katika vituo vya afya nchini kwa kuzingatia weledi unaojali utu na misingi ya maadili ya utabibu.

Akizungumza kuhusu tukio hili, Msemaji Mkuu wa Serikali alisisitiza kuwa vitendo hivyo ni hatari hasa kwa kuzingatia hali ya sasa nchini.

Kupitia taarifa yake, Msemaji Mkuu alisema: “Kwa wakati huu ambapo Watanzania tumepitia madhira yaliyosababishwa na vurugu za tarehe 29 Oktoba, 2025 sio busara kuchochea taharuki kwa watu kwa kutengeneza picha zenye kutia uchungu na hasira kwa watu.”

Alionya vikali kuwa wale wanaofanya vitendo hivi sio tu wanachafua nchi, bali pia wanavunja Sheria za nchi na kusababisha hofu isiyo ya lazima kwa umma na kutoa wito kwa Watanzania wote kuacha mara moja vitendo vya kutengeneza na kusambaza habari au picha za upotoshaji. 

Aidha aliutaka umma kuwa makini na taarifa za uongo (fake news) zinazochochea chuki, hasira, na kuvuruga amani ya nchi.



Post a Comment

Previous Post Next Post