" TUMUUNGE MKONO RAIS KATIKA KUREJESHA AMANI NA UTULIVU

TUMUUNGE MKONO RAIS KATIKA KUREJESHA AMANI NA UTULIVU

 Baada ya uchaguzi mkuu kufanyika na viongozi kuchaguliwa kihalali, Tanzania inajikuta katika kipindi muhimu cha mtihani wa amani, utulivu, na upendo wa wananchi wake. Huku jitihada za Serikali zikilenga uponyaji na maridhiano, wapo baadhi ya watu wanaendeleza vitendo vya kuchochea vurugu kwa maslahi yao binafsi.

Kiongozi Mkuu wa Nchi, Dk Samia Suluhu Hassan alipozindua Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alitoa hotuba ya faraja iliyorejesha matumaini kwa Watanzania. Hotuba hiyo ilibeba mwelekeo wa hatua za kuleta amani ya kudumu, ikiwemo: akizungumzia uundwaji wa Tume ya kufanya uchunguzi wa kina kuhusu vurugu zilizotokea nchini;Kuangaliwa upya kwa mashtaka kwa wale waliokamatwa kutokana na kusababisha vurugu, kwa lengo la kuwasamehe;Kuimarisha amani na mshikamano kupitia mchakato wa maridhiano utakaosimamiwa na Kiongozi Mkuu na Kuanzisha mchakato wa Katiba mpya kwa ajili ya mustakabali bora wa Taifa.

Hatua hizi zimepokelewa kwa furaha kubwa na Watanzania wengi, ambao wanatamani kurudisha utamaduni wa kuishi kwa amani na mshikamano ambao ndio asili yao.

Uhujumu Amani kwa Maslahi ya Wafanyabiashara

Licha ya jitihada hizi za kiserikali, kuna baadhi ya watu – ikiwemo wafanyabiashara wanaoishi nje ya nchi – ambao wanaendeleza vitendo viovu vinavyolenga kuvuruga amani yetu.

Watu hawa wanadaiwa kuchochea vurugu na uharibifu wa mali za umma na binafsi kabla na wakati wa uchaguzi, wakitumia kauli mbiu za uhamasishaji zilizopelekea maafa yasiyosimulika kwa Watanzania.

Inaripotiwa kuwa vurugu hizi zimekuwa 'biashara' inayowaingizia pesa wachache, huku wakiungwa mkono na makundi ya kisiasa yanayotaka kupata madaraka kwa mgongo wa mateso ya Watanzania kwa kukwepa kushiriki uchaguzi. Matendo yao maovu yanaendelea kwa kueneza lugha za chuki na kuchochea vurugu mpya kwa tarehe zijazo.

 "Ndugu zangu Watanzania, tusikubali kulishwa ujinga huu ambao ulipelekea majanga makubwa katika nchi jirani. Tangu lini Watanzania tukawa na chuki za namna hii? Tuliendelee kulinda amani yetu. Bila amani, hakuna elimu, hakuna biashara wala hakuna furaha."

Viongozi wa Dini wanapaswa kuendelea kutumia nafasi zao kuwatoa wananchi kwenye mtanziko huu wa kiusalama unaosababishwa na chuki zinazopandikizwa. Hakuna mshindi katika 'mashindano' haya ya vurugu, bali Taifa zima linaoishi Tanzania ndilo linapata hasara kwa kupoteza watoto, mali, na kuporomoka kwa uchumi.

Tanzania ni Yetu Sote: Tusikubali kubomoa nchi yetu kwa uchochezi wa watu wasioishi Tanzania. Kesho bora ya Tanzania itajengwa kwa kuendelea kuenzi amani, kuvumiliana na kushirikiana.


Post a Comment

Previous Post Next Post