Na: Dkt. Reubeni Lumbagala, Misalaba Media
Je, unatamani kufanya Mtihani wa Taifa Kidato cha Sita (ACSEE) ukiwa kama Mtahiniwa wa Kujitegemea (Private Candidate)? Kama jibu ni ndiyo, basi nafasi bado ipo. Ndiyo, nafasi ya kukamilisha usajili ipo, ni wewe tu kuichangamkia fursa hii.
Iko hivi: Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) limeongeza muda wa usajili kwa Watahiniwa wa Kujitegemea wa Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Sita (ACSEE) kwa mwaka 2025 kutoka Novemba 6, 2025 hadi Novemba 30, 2025.
Hii inatokana na Taarifa iliyotolewa Novemba 6, 2025 na Katibu Mtendaji wa NECTA, Prof. Said Mohamed, ambapo hamasa imetolewa kwa wale wote wenye dhamira ya kufanya mtihani wa ACSEE wakiwa kama Watahiniwa wa Kujitegemea kutumia vyema muda ulioongezwa wa hadi Novemba 30, 2025 ili kukidhi vigezo vya kufanya mitihani hiyo inayotarajiwa kufanyika mwakani. Aidha, waombaji wanapaswa kulipia gharama ya Shilingi 65,000 ikiwa ni ada ya usajili.
Ikumbukwe NECTA imeweka utaratibu wa kuruhusu Watahiniwa wa Kujitegemea nje na mfumo rasmi wa shule kuweza kujisajili na kufanya mitihani ya Taifa ikiwa ni malengo ya serikali ya kutanua wigo kwa wananchi kupata elimu katika mifumo mbalimbali ili kutimiza malengo yao kielimu na ya kimaisha.
Kimsingi, yapo mazingira ambayo pengine kwa namna moja au nyingine, mwombaji akawa ameshindwa kukamilisha usajili wake kama Mtahiniwa wa Kujitegemea wa Kidato cha Sita. Kwa kuzingatia mazingira ya aina hii, NECTA wameongeza muda ili kila mwenye dhamira ya kujisajili aweze kufanikisha dhamira yake hiyo njema.
Nami naungana na NECTA kuwahimiza wale wote ambao hawajajisajili kutumia vyema muda huu wa nyongeza ili kukamilisha usajili wao ili waweze kukidhi vigezo vya kufanya mitihani hiyo hapo mwakani.
Dkt. Reubeni Lumbagala ni Mwalimu wa Shule ya Sekondari Funguni ya wilayani Pangani mkoani Tanga.
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA

Post a Comment