
Na Fabius Clavery, Misalaba Media-Kagera.Askofu wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Jovitus Francis Mwijage amewataka Wakristu na Watanzania wote kutumia kipindi hiki cha Tafakari ya Kuzaliwa Bwana Yesu Kristu kuunganika kama familia moja na kuondoa tofauti zao.Ameyasema hayo katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Mkesha wa Kuzaliwa Bwana Yesu Kristo Disemba 24 Kanisa Kuu, Parokia ya Bukoba Jimbo Katoliki la Bukoba.Askofu Mwijage amesema jamii itafakari kuondoa makovu yaliyojitokeza kutokana na matukio ya Uchaguzi kwa kuondoa ubabe, kukubali ukweli, kuacha propaganda na uanaharakati huku akishauri tukio lililotokea na kupoteza maisha ya watu na mali lijengewe alama ya kumbukumbu ili vizazi vinavyokuja visilete mzaha juu ya masuala ya Haki na Amani.Aidha, amewataka watu wote kuheshimu Haki na Utu wa mtu huku akiwanasihi wale waliopewa dhamana ya kusimamia hayo kutojiingiza katika vitendo vya kudhalilisha Haki na Utu wa mtu yeyote."Tunahitaji kuwa Wanyenyekevu kila mmoja kwa nafasi yake".Kdhalika Askofu Mwijage amewataka wazazi na walezi katika familia kujenga utamaduni wa kuomba msamaha pale mmoja anapokosea ndipo watoto wataweza kujifunza kwao na nyumba kuwa na amani. Aidha, amewata viongozi wa kijamii kuwa na utamaduni wa kuomba msamaha pale yanapotokea makosa kwakua jamii haitawaliki kwa tabia ya kiburi.




Post a Comment