" DKT. MWIGULU ACHEFUKWA, AWAFUTA KAZI WATUMISHI TEMESA

DKT. MWIGULU ACHEFUKWA, AWAFUTA KAZI WATUMISHI TEMESA




DAR ES SALAAM;

Waziri Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba, ameagiza kuchukuliwa hatua za haraka dhidi ya watumishi wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) waliobainika kuhusika na ubadhirifu wa fedha za umma kiasi cha Sh bilioni 2.5, akisisitiza kuwa hatua hiyo ni muhimu kulinda rasilimali za Taifa na kuboresha huduma za usafiri wa vivuko kwa wananchi.

Dk. Mwigulu ametoa agizo hilo leo Desemba 24, 2025, alipofanya ziara ya kukagua utendaji wa kivuko katika eneo la Kigamboni jijini Dar es Salaam, ambapo amesema ubadhirifu wa fedha umekuwa miongoni mwa sababu kuu zinazosababisha kudorora kwa huduma za vivuko na kuongezeka kwa gharama zisizo za lazima kwa serikali.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Waziri Mkuu amesema vitendo vya matumizi mabaya ya madaraka na fedha za umma vinapaswa kukomeshwa ili kurejesha ufanisi na uwajibikaji katika taasisi za umma, akionya kuwa watumishi wanaokiuka maadili ya utumishi hawana nafasi katika Serikali.

“Watu wasioweza kujirekebisha ni lazima warekebishwe. Kumekuwepo na matumizi mabaya ya madaraka na fedha, hali ambayo haiwezi kuvumiliwa,” amesema Dk. Mwigulu.

Ameeleza kuwa kwa sasa baadhi ya vivuko vimeshindwa kufanyiwa matengenezo kutokana na kuwepo kwa madeni yanayofikia takribani Sh milioni 800, huku taarifa za kifedha zikionesha kuwa baadhi ya watumishi wa TEMESA wamehusika moja kwa moja na ubadhirifu wa Sh bilioni 2.5.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, hali hiyo imesababisha serikali kubebeshwa mzigo mkubwa wa kifedha, jambo linaloathiri mipango ya kuboresha au kununua vivuko vipya vinavyoweza kutoa huduma bora, salama na ya uhakika kwa wananchi.

Dk. Mwigulu ameonya kuwa endapo hatua kali hazitachukuliwa mapema, serikali inaweza kuendelea kutumia fedha nyingi katika matengenezo ya vivuko chakavu badala ya kuelekeza rasilimali hizo kwenye uwekezaji wa vivuko vipya, hali itakayoongeza mzigo kwa wananchi na kudhoofisha utoaji wa huduma muhimu za usafiri.

Post a Comment

Previous Post Next Post