Na Lydia Lugakila, Misalaba Media MbeyaBaadhi ya wakazi wa Mkoa wa Mbeya wameipongeza Hifadhi ya Wanyama porina makumbusho ya IFISI Zoo and Game Farm, iliyopo Kijiji cha Ukumbi, mtaa wa Ifisi katika mji mdogo wa Mbalizi, kwa uwekezaji na huduma wanazotoa katika kukuza utalii wa ndani, hasa kwa kuwawezesha watoto kuona na kujifunza kuhusu wanyama kwa karibu.Wazazi ambao pia ni walimu kutoka Shule ya Isaiah Samaritan International ya Isyese, Bi Hollo Mbisa na Hamza Abdul, wamesema kuwa hifadhi hiyo imekuwa chachu ya maendeleo ya elimu kwa watoto kwani imewawezesha kujifunza kwa vitendo. Wameeleza kuwa kwa muda mrefu wamekuwa wakifundisha darasani bila wanafunzi kuona wanyama halisi, hivyo ziara hizo zimewasaidia kufahamu tabia na sifa za wanyama kwa upeo mpana zaidi.Wazazi hao wamewahamasisha wazazi wenzao kujenga utamaduni wa kupeleka watoto katika maeneo kama hayo ili kujifunza mambo mbalimbali, ikiwemo mali kale na historia za nchi.Kwa upande wake, Meneja wa IFISI Zoo and Game Farm, Bi Veronica Jacob, amesema kuwa hifadhi hiyo imekuwa mwarobaini wa elimu ya utalii kwa watoto wengi, kwani imeandaliwa kutoa maarifa ya kutosha kuhusu wanyama na urithi wa utamaduni.Ameeleza kuwa hifadhi hiyo inatoa fursa ya kuona wanyama waliopo mabandani, wanyama walio nje ya mabanda, pamoja na jumba la makumbusho lenye historia adhimu.Miongoni mwa wanyama waliopo ni Simba, Fisi, Nungunungu, Mamba, Nyoka aina ya Mlalwe, Kifutu, Chatu, Swala wakubwa, Pundamilia, Nyumbu pamoja na wanyama wengine.Amesema kuwa katika jumba la makumbusho, wageni wanaweza kujionea vitu kama mikuki ya kale, fedha zilizotumika kabla na baada ya ukoloni, pesa za Wajerumani na Waingereza, mafuvu ya wanyama, mishale, pamoja na farasi wa baharini.Bi Jacob amewakaribisha wakazi wa Mbeya na nje ya mkoa huo kutembelea hifadhi hiyo hususan katika msimu huu wa sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya, akisisitiza kuwa ni fursa muhimu kwa watoto kupata elimu kupitia utalii wa ndani.Aidha, amesema kuwa kwa msimu huu IFISI Zoo imejipanga kikamilifu kuwapokea wageni, huku ikijivunia gharama nafuu zinazowezesha watu wote kumudu na kufurahia vivutio vilivyopo.









Post a Comment