" TAKWIMU: JKCI YAONYA HATARI YA VIFO VYA GHAFLA KWA WANAMICHEZO, YAANZISHA HUDUMA MAALUM ZA UCHUNGUZI WA AFYA YA MOYO

TAKWIMU: JKCI YAONYA HATARI YA VIFO VYA GHAFLA KWA WANAMICHEZO, YAANZISHA HUDUMA MAALUM ZA UCHUNGUZI WA AFYA YA MOYO

 Takwimu za shirika la National Collegiate Athletic Association (NCAA) za mwaka 2024 zinaonesha kuwa kati ya wanamichezo 50,000 mmoja yupo katika hatari ya kudondoka na kupoteza maisha ghafla kutokana na matatizo ya moyo yanayotokana na sababu za kuzaliwa au mabadiliko yanayojitokeza baada ya kushiriki michezo kwa muda mrefu.

Hayo yameelezwa na Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group Eva Wakuganda wakati wa zoezi la uchunguzi wa afya ya moyo kwa wanamichezo wanaoshiriki mashindano ya 16 ya chipkiz cup katika viwanja vya Tanganyika Game Trackers (TGT) mkoani Arusha.

Dkt. Wakuganda amesema kuwa kutokana na changamoto hizo Taasisi ya moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imeanzisha kitengo maalum cha kutoa huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo kwa wanamichezo ndani nan je ya nchi.

“Hiki ni kitu muhimu sana ambacho kama Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete tumekianzisha ili kuwafikia wanamichezo wa ngazi mbalimbali kuanzia timu za taifa, vilabu mbalimbali, michezo ya aina zote, wanamichezo wanaofanya mazoezi katika gym pamoja na wanafunzi mashuleni”. Alisema Wakuganda.

Ameeleza kuwa kwa wanamichezo wote waliokuja kufanya uchunguzi na matibabu ya moyo wamepewa ushauri wa kitaalamu ikiwemo dalili za hatari wanazopaswa kuzingatia na umuhimu wa kufanya uchunguzi wa mara kwa mara wa afya ya moyo.

Dkt. Wakuganda ametoa wito kwa wanamichezo wote nchini Tanzania kutumia fursa hiyo kwa kufika Tasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa ajili ya uchunguzi na matibabu ya moyo.

“Kwa sasa tunakaribisha wanamichezo wote kuja kupima afya zao ili kubaini uwezo wao wa kimwili kuboresha utendaji na kuzuia vifo vya ghafla vinavyoweza kuzuilika”. Alisema Dkt. Wakuganda.

Kwa upande wake Kocha wa Kibera Agoal Academy kutoka Kenya Emmanuel Ouma ameishukuru Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa huduma walizotoa kwa wanamichezo, amesema kuwa huduma hizo ni muhimu sana katika kuzuia vifo vya ghafla uwanjani.

“Nimeshuhudia kwa macho yangu mwanamichezo mwenzangu akifariki uwanjani kwasababu hajawahi kufanya uchunguzi na matibabu ya moyo, ndiyo maana ninashukuru sana JKCI kwa kazi kubwa wanayoifanyakwani inasaidia walimu na makocha kufahamu hali ya afya za wachezaji wetu”.  Alisema Ouma.

Naye mchezaji wa Arusha Youth Development Organization Academy Hossian Lowasa amesema zoezi la kupima afya ya moyo limemsaidia kufahamu hali yake ya kiafya.

“Nimeshauriwa kuendelea kufanya mazoezi kwa usahihi kuzingatia lishe bora na kula matunda ili kulinda afya ya mwili wangu”. Alisema Hossiana.

Kwa upande wakemchezaji wa Kibera Agoal Academy kutoka Kenya Labida Basmi amesema ameridhishwa na huduma za afya zilizotolewa na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).

“Nimefurahi sana kushiriki mashindano haya na kupata huduma nzuri za afya, nawashukuru sana wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa huduma wanazotupatia”. Alisema Basmi.

Mashindano haya ya 16 ya Chipkiz cup yanaendelea kufanyika mpaka tarehe 21 Desemba 2025 katika viwanja vya Tanganyika Game Trackers (TGT) mkoani Arusha, na kuuhudhuriwa na wanamichezo kutoka nchi tofauti kama vile Tanzania, Kenya, Uganda na Zimbabwe


Post a Comment

Previous Post Next Post