" ULINZI WAIMARISHWA KUELEKEA SIKUKUU ZA MWISHO WA MWAKA MKOANI MBEYA

ULINZI WAIMARISHWA KUELEKEA SIKUKUU ZA MWISHO WA MWAKA MKOANI MBEYA






Kuelekea sikukuu za mwisho wa mwaka, 2025 Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limejipanga vizuri kuhakikisha ulinzi na usalama wa raia na mali zao unaimarishwa kwa kufanya misako na doria za Magari, Pikipiki, Miguu na kwa kutumia Wanyama kazi Mbwa wa Polisi kuzuia na kudhibiti uhalifu.

Aidha, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limejipanga vizuri kuzuia na kudhibiti makosa ya usalama barabarani kwa kufanya doria katika barabara kuu ya TANZAM, kufanya ukaguzi wa magari katika maeneo rasmi ya vizuizi, Iwambi, Inyala na Shamwengo pamoja na kutumia vifaa vya kisasa vya kupimia kilevi na “speed rader” ili kuzuia ajali zinazosababishwa na uzembe.

Sambamba na hayo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawataka wananchi kuhakikisha wanaacha waangalizi kwenye makazi yao pindi wanapotoka kwenda kwenye misa na ibada za mkesha, wanapokwenda kusheherekea na kwenye matamasha hasa wakati wa usiku ili kuepuka matukio ya uhalifu katika makazi yao.

Pia, wazazi na walezi wana kumbusha kulipa kipaumbele suala la ulinzi na usalama wa mtoto kwa kuhakikisha watoto wanaongozana na watu wazima wanapo kwenda ibadani au kusherehekea katika maeneo mbalimbali hasa yenye mikusanyiko ya watu ili kuepuka kupotea na kuwawezesha katika kuvuka salama barabara, kurudi nyumbani na kuwaepusha na mazingira na vitendo hatarishi.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linapiga marufuku mtu yeyote kupiga/kulipua milipuko [Fataki] bila kuwa na kibali cha Jeshi la Polisi.

Watakaopiga Fataki ni wale walioomba na kupata kibali kwa ajili ya kupiga fataki katika sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya. Aidha, kila aliyepata kibali anatakiwa kuzingatia masharti na vigezo vya usalama katika ulipuaji/upigaji wa Fataki.

Kwa maeneo yenye fukwe kama vile Matema, Ngonga – Wilaya ya Kyela, Kisiba – Wilaya ya Rungwe na Ziwa Ngosi, ulinzi umeimarisha na tunawataka wamiliki wa maeneo hayo kuweka walinzi na waangalizi kwani katika kipindi hiki tunategemea watu wa rika tofauti kwenda katika maeneo hayo.
Wamiliki wa kumbi za starehe pia wanatakiwa kuhakikisha wanaweka walinzi binafsi katika maeneo ya ndani na nje ya kumbi hususani kwenye maegesho ya magari ili kuzuia uhalifu kama vile wizi.

Kuhakikisha wanajua uwezo wa kumbi zao ili kuepuka kuzidisha watu na kusababisha madhara ya kibinadamu.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linatoa wito kwa makundi yote ya kijamii kuhakikisha yanazingatia suala la utii wa sheria bila shuruti na kujiepusha na vitendo vya kihalifu au uvunjifu wa amani wa namna yoyote ile.

Aidha, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linatoa rai kwa wananchi kuendelea kushirikiana kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi ya wahusika.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawatakia wananchi wote wa Mkoa wa Mbeya maandalizi mema ya Sikukuu ya Krismasi na Mwaka mpya 2026.

Post a Comment

Previous Post Next Post