
Na Sophia Kingimali
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, Joel Arthur Nanauka, amesema Serikali ya Awamu ya Sita imejipanga kikamilifu kuwawezesha vijana kiuchumi na kijamii kwa kuwafikia walipo, kuwasikiliza na kuwashirikisha katika kupanga na kutekeleza mipango ya maendeleo ya Taifa.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Desemba 23, 2025, jijini Dar es Salaam, Nanauka amesema vijana ni rasilimali kubwa ya Taifa, akitaja takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 zinazoonesha kuwa vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 35 ni zaidi ya milioni 20.6, sawa na zaidi ya asilimia 55 ya nguvu kazi ya nchi.
“Mwelekeo wa Serikali ni kuifuata dira ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuongeza ajenda ya ajira, ujuzi, uzalishaji na matumizi ya teknolojia, ili vijana wanufaike na fursa za uchumi wa sasa na wa baadaye,” amesema Nanauka.
Waziri Nanauka amesema hatua hizo zinaendana na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 pamoja na Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2025–2030, inayolenga kuzalisha ajira zisizopungua milioni nane ndani ya kipindi cha miaka mitano ijayo.
Aidha, ametaja changamoto kuu zinazowakabili vijana kuwa ni ukosefu wa ajira zenye staha, upungufu wa ujuzi unaohitajika sokoni pamoja na ukosefu wa mitaji kwa vijana wajasiriamali na kampuni changa, akisema Serikali imejipanga kukabiliana nazo kupitia sera na mikakati mbalimbali.
Nanauka amesema Serikali itaendelea kuimarisha utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana ya mwaka 2007, toleo la 2024, kwa kuzingatia maeneo 13 ya kipaumbele ikiwemo elimu ya ufundi stadi, uchumi wa kidijitali, ubunifu, uongozi, afya, usawa wa kijinsia na ujumuishwaji wa vijana wenye ulemavu.
Akizungumzia ajira, amesema Serikali inaandaa mikakati ya kuongeza fursa za kazi ndani na nje ya nchi, kuimarisha huduma za ajira na kulinda haki za vijana wanaoajiriwa nje ya nchi, sambamba na kuendeleza programu za mafunzo kazini na uzoefu wa kazi kupitia mifuko ya maendeleo ya ujuzi.
Ameongeza kuwa Serikali inawekeza katika sekta zenye ajira nyingi ikiwemo kilimo-biashara, madini, uvuvi na viwanda, pamoja na kuimarisha uwekezaji kupitia kongani na maeneo maalumu ya kiuchumi ili kuongeza ajira na ujuzi kwa vijana.
Katika kuwezesha mitaji, Waziri Nanauka amesema Serikali imeanza kuimarisha mifumo ya dhamana ya mikopo ili kuwasaidia vijana wengi wanaokosa dhamana kupata mikopo, pamoja na kusimamia kutengwa kwa asilimia 30 ya ununuzi wa umma kwa makundi maalumu ikiwemo vijana.
Ameongeza kuwa Serikali itaandaa pia jukwaa la kidijitali la huduma jumuishi kwa vijana (Youth Digital One Stop Platform) litakalowaunganisha vijana na taarifa za ajira, mafunzo, mikopo na masoko, kama sehemu ya kutumia teknolojia kurahisisha upatikanaji wa huduma.
Nanauka ameeleza kuwa Serikali itaendelea kuimarisha majukwaa ya ushiriki wa vijana kama VIJANA Platform, pamoja na kufufua vituo vya maendeleo ya vijana vya Sasanda, Ilonga na Marangu ili kutoa ujuzi wa vitendo, nidhamu na stadi za ujasiriamali.
Amewataka vijana wa Tanzania kuwa wazalendo, wachapakazi na wenye nidhamu, wakilinda amani na mshikamano wa Taifa, huku akisisitiza kauli mbiu ya “Vijana Tuyajenge, Tanzania ni Yetu,” akiahidi kuwa ofisi yake iko wazi kwa ajili ya kusikiliza na kuhudumia vijana wote.

🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254
Post a Comment