" WAZIRI SANGU ATETA NA VIONGOZI WA MAKANISA YA KIPENTEKOSTE (CPCT)

WAZIRI SANGU ATETA NA VIONGOZI WA MAKANISA YA KIPENTEKOSTE (CPCT)

Na: OWM – KAM, Dar es Salaam

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mheshimiwa Deus Clement Sangu(Mb.), amekutana na kufanya mazungumzo na Viongozi wa Baraza la Maaskofu wa Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (CPCT) Disemba 20, 2025, Jijini Dar es Salaam.

Lengo la kukutana na viongozi hao ni kujitambulisha na kuelezea jukumu jipya la mahusiano ambalo Ofisi yake imepewa kuliratibu kufuatia Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kuunda Wizara inayohusu kujenga mahusiano baina ya Serikali na wadau wa makundi mbalimbali ya kijamii, kisiasa, kiuchumi, kikanda na Kimataifa.

Katika kikao hicho Waziri Sangu alisema mahusiano ni mchakato shirikishi, endelevu wa mawasiliano ya pande mbili au zaidi ambao unalenga kuwaleta pamoja na kuwawezesha wananchi na wadau kushiriki kikamilifu katika kutoa maoni, kushirikishwa katika maamuzi, kufuatilia utekelezaji wa Sera na Programu za Serikali ili kujenga uwajibikaji kwa ajili ya maendeleo ya Taifa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu wa Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (CPCT), Askofu Vernon Fernandes amesema wataendelea kushirikiana na Serikali katika kusaidia jamii kiroho, kuimarisha mshikamano na kuunga mkono juhudi za maendeleo nchini.

Askofu Fernandes alishukuru kitendo cha Waziri Sangu kwenda kuwatembelea na kuzungumza nao ambapo aliongeza kusema ni hatua nzuri za Serikali kukuza mahusiano na Taasisi za dini pamoja na wananchi .

Katika kikao hicho, Waziri Sangu aliambatana na Wakurugenzi na Maafisa waandamizi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano. Mhe. Waziri alipata wasaa wa kusikiliza ushauri na maoni ya Viongozi wa Baraza la Maaskofu wa CPCT kwa lengo la kubainisha maeneo yanayohitaji kuimarishwa katika masuala ya mahusiano nchini.

Post a Comment

Previous Post Next Post