" Askofu Ruwaichi Asisitiza Wakristo Feki Wapuuzwe

Askofu Ruwaichi Asisitiza Wakristo Feki Wapuuzwe

 

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi, amewatahadharisha walezi na wazazi kuwapuuza vijana wanaojigamba kuwa ni Wakristo huku wakikashifu kanisa, akieleza kuwa imani ya watu hao ni “feki” na haina mizizi.

Kauli hiyo ameitoa hivi karibuni katika Parokia ya Mtakatifu Gaspar-Mbezi Beach, wakati wa Adhimisho la Misa Takatifu ya Shukrani kwa ajili ya walezi wa Shirika la Kipapa la Utoto Mtakatifu Jimbo. Kwa mujibu wa Gazeti Tumaini Letu, Askofu Ruwa’ichi amebainisha kuwa chimbuko la vijana hao kukashifu imani yao ni ukosefu wa misingi imara ya malezi tangu utotoni.

“Zama hizi za sasa wanajitokeza vijana na kujigamba wao ni Wakristo, lakini wamekuwa wakiuchimbia mwili na Ukristo wenyewe, japo kama ni kweli, kwanini wanauchimbia mwili na Ukristo? Na hao Ukristo wao ni ‘feki’, na hauna mizizi wala kina, alisema Askofu Mkuu Ruwa’ichi.

Askofu Mkuu amesisitiza kuwa malezi yaliyotengemaa yanahitaji uwepo wa wazazi wote wawili (mama na baba), kwani uwepo wa mzazi mmoja pekee unaweza kusababisha “ulemavu wa kiroho” katika ukuaji wa mtoto. Aidha, amewakumbusha walezi kuzingatia tofauti za kisaikolojia kati ya watoto wa kiume na wa kike tangu wakiwa wadogo.

Askofu Mkuu Ruwa’ichi alisema kwamba, malezi yaliyotengemaa yanamhitaji mama na baba, kwa sababu uwepo wa watu hao huleta hali nzuri ya kutengemaa, na kuwepo kwa mzazi mmoja kuna hatari kubwa ya kulemaa kwa familia.

Kwa mujibu wa Askofu Mkuu Ruwa’ichi, wanadamu wamejaliwa tunu mbalimbali, ambazo nyingine huitwa fadhila, japokuwa kuna maelekeo mengine yanaweza yakaitwa ni uovu au ulemavu.

Aliendelea kusema kwamba, kuna baadhi ya tunu zinaweza kusifiwa kama ni fadhila, ambazo ni upendo, urafiki, utu wema na huruma, japokuwa huwa haziji zenyewe, bali ni kwa sababu ya malezi bora.

Askofu huyo, aliwasisitiza walezi wafahamu kuwa, mtoto asipolelewa wala kurithishwa tunu zilizo bora, anakuwa mlemavu, japo siyo wa viungo bali ni wa roho, na anaweza kuumiza zaidi kuliko hata yule wa viungo.

Katika homilia yake, Askofu ameeleza kuwa fadhila kama upendo, urafiki, utu wema, na huruma haziji kwa bahati mbaya, bali ni matunda ya malezi bora.

Post a Comment

Previous Post Next Post