" CCM BUKOBA MJINI YAKABIDHI MSAADA KWA VITUO VYA WATOTO YATIMA KUELEKEA MAADHIMISHO YA MIAKA 49 YA CHAMA

CCM BUKOBA MJINI YAKABIDHI MSAADA KWA VITUO VYA WATOTO YATIMA KUELEKEA MAADHIMISHO YA MIAKA 49 YA CHAMA



‎Fabius Clavery, Misalaba Media-Kagera.

‎Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Bukoba Mjini kimekabidhi msaada wa vituo mbalimbali kwa vituo viwili vya kulelea watoto yatima vya Hamugembe na Kashai, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 49 ya kuasisiwa kwa chama hicho tawala nchini.
 ‎
Msaada uliokabidhiwa katika vituo hivyo unajumuisha mahitaji muhimu ya kila siku ikiwemo mchele, sukari, unga, sabuni, pamoja na vifaa vya shule kama vile madaftari, kalamu na penseli, kwa lengo la kusaidia ustawi na maendeleo ya watoto wanaolelewa katika vituo hivyo. ‎

Akizungumza mara baada ya kukabidhi msaada huo, Katibu wa CCM Wilaya ya Bukoba Mjini, Shaban Mdohe, amesema chama hicho kinatambua mchango mkubwa unaotolewa na vituo vya watoto yatima katika jamii, na hivyo kuahidi kuwa Serikali ya Wilaya itakwenda kuzifanyia kazi changamoto mbalimbali zilizoainishwa na viongozi wa vituo hivyo. 

‎Miongoni mwa changamoto hizo ni ukosefu wa bima ya afya kwa watoto, hali inayosababisha ugumu wa upatikanaji wa huduma za afya pale wanapougua. ‎

Ameeleza kuwa katika kuadhimisha miaka 49 ya CCM, chama hicho kimepanga kuendelea na shughuli mbalimbali za kijamii, zikiwemo upandaji wa miti, uchangiaji wa damu, pamoja na kufanya usafi wa mazingira, kama sehemu ya kuimarisha mshikamano na kutoa mchango chanya kwa jamii. 

Kwa upande wake mstahiki meya wa Manispaa ya Bukoba Ackton Rwankomezi ameahidi kuhakikisha wanatekeleza maelekezo ya chama hicho wakati wote.

‎CCM imeendelea kusisitiza dhamira yake ya kushiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii kama sehemu ya utekelezaji wa falsafa ya kujali watu na maendeleo ya jamii kwa ujumla. ‎






Post a Comment

Previous Post Next Post