" CHILOMBE ATOA ONYO: WELEDI NA UPENDO NI MSINGI HUDUMA ZA AFYA TUNDURU

CHILOMBE ATOA ONYO: WELEDI NA UPENDO NI MSINGI HUDUMA ZA AFYA TUNDURU

Na Mwandishi wetu, Misalaba MediaWatumishi wa sekta ya afya wilayani Tunduru wameaswa kufanya kazi kwa weledi, upendo, uadilifu na kujitoa katika kuwahudumia wagonjwa, hatua inayolenga kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa wananchi na kuimarisha imani ya jamii kwa mifumo ya huduma za umma.Rai hiyo imetolewa na Mbunge wa Jimbo la Tunduru Kusini, Mhandisi Fadhili Chilombe, alipokuwa akizungumza na watumishi wa sekta ya afya katika mkutano uliofanyika kwenye ukumbi wa Hospitali ya Wilaya ya Tunduru, ikiwa ni sehemu ya ziara zake za kusikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili watoa huduma.Chilombe aliwataka watumishi kuzingatia vipaumbele vya sekta ya afya ikiwemo kutoa huduma kwa haki bila upendeleo, kuheshimu wagonjwa, kuzingatia maadili ya taaluma, kuwajibika kazini na kushirikiana ili kulinda maisha na ustawi wa wananchi.Ili kupata picha halisi ya changamoto zilizopo, Mbunge huyo aliweka utaratibu wa kukusanya maoni na changamoto za watumishi kwa njia ya maandishi kwa usiri bila kutaja majina, hatua aliyosema itasaidia kubaini tatizo halisi na kwa lengo la kubaini changamoto za kiutendaji na kuja na suluhu zitakazoleta mabadiliko chanya katika hali ya utoaji wa huduma za afya.Akiambatana na baadhi ya madiwani wa kata, Chilombe amesema yapo malalamiko kutoka kwa watumishi yanayohusiana na ukosefu wa uadilifu kwa baadhi ya viongozi, hali inayopunguza morali ya kazi, huku pia kukiwa na malalamiko kutoka kwa wananchi yanayotokana na uzembe wa baadhi ya watoa huduma.Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru, Hassan Dauda, amesema utoaji wa huduma za afya wilayani humo unakabiliwa changamoto za upotevu wa ukusanyaji mdogo wa mapato ya ndani unaoathiri upanuzi wa huduma kwa jamii, pamoja na uhaba wa watumishi wa kada mbalimbali katika baadhi ya vituo.Awali, akitoa taarifa ya hali ya utoaji wa huduma za afya wilayani Tunduru, Kaimu Mkuu wa Idara ya Afya, Ustawi wa Jamii na Huduma za Lishe, Renatus Mathias, amesema uhaba wa watumishi unasababisha baadhi yao kufanya kazi kwa muda mrefu zaidi ya saa zilizopangwa, hali inayochangia kuchoka na wakati mwingine kushuka kwa ubora wa huduma.Ameeleza kuwa licha ya changamoto hizo, uongozi wa wilaya unaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuboresha mazingira ya kazi na huduma za afya, akisisitiza kuwa ushirikiano kati ya watumishi, viongozi na wananchi ni msingi wa kuimarisha sekta ya afya na kuhakikisha wananchi wa Tunduru wanapata huduma bora, salama na zenye heshima.



 

 

Post a Comment

Previous Post Next Post