" DC CHIKOKA AONGOZA KAMPENI YA "MTI WA MAMA" MUSOMA, MITI 150 YAPANDWA

DC CHIKOKA AONGOZA KAMPENI YA "MTI WA MAMA" MUSOMA, MITI 150 YAPANDWA


MUSOMA MARA.

Mkuu wa Wilaya ya Musoma Mkoani Mara, Juma Chikoka, amewaongoza watumishi wa serikali, walimu pamoja na wanafunzi wa Manispaa ya Musoma kupanda miti zaidi ya 150 katika Shule ya Kigera Mwiyale. Zoezi hilo limefanyika ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya kumbukizi ya siku ya kuzaliwa ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, yenye kaulimbiu ya “Miaka 27 ya Kijani – Mti wa Mama.”

Shughuli hiyo imeandaliwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa lengo la kuhakikisha utekelezaji wa kaulimbiu hiyo, ambapo wameeleza kuwa zoezi hilo ni sehemu ya jitihada za kuendeleza na kutunza mazingira kwa kupanda na kulinda miti.

Akizungumza katika zoezi hilo, Mkuu wa Wilaya Juma Chikoka amesema kuwa utunzaji wa mazingira ni wajibu wa kila mwananchi, na kutoa rai kwa wakazi wa Wilaya ya Musoma kuwa na utamaduni wa kupanda miti na kuilinda hadi ifikie hatua ya kukua.

Aidha, amewataka wananchi wote wanaoharibu mazingira kwa kukata miti hovyo pamoja na wale wanaojihusisha na shughuli zinazosababisha uharibifu wa mazingira, kuacha mara moja vitendo hivyo kwa ajili ya kulinda mazingira na vizazi vijavyo.




Post a Comment

Previous Post Next Post