Na Lydia Lugakila -Misalaba media
Chunya, Mbeya.
Mkuu wa Idara ya Elimu ya Awali na Msingi, Mwalimu Marko I. Busungu, amewataka walimu waliopatiwa vifaa visaidizi kuhakikisha wanavitunza kwa uangalifu ili viweze kudumu na kuwasaidia kwa muda mrefu katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Mwalimu Busungu ametoa wito huo mapema leo, Januari 27, 2026, katika Ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Chunya, wakati wa zoezi la kukabidhi vifaa hivyo kwa walimu wenye mahitaji maalum, ili waanze kuvitumia kama Serikali ilivyoelekeza.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mwalimu Busungu amesema kuwa kutunza vifaa hivyo ni ishara ya kuthamini juhudi za Serikali pamoja na kumtendea haki Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dokta Samia Suluhu Hassan ambaye ndiye aliyeridhia upatikanaji wa vifaa hivyo kwa ajili ya kuwasaidia walimu katika utendaji kazi wao.
“Naomba nitoe rai kwa walengwa wa vifaa hivi wavihudumie na kuvitunza vizuri ili viweze kutumika kwa muda mrefu kwa kufanya hivyo mtakuwa mmemtendea haki Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwani yeye ndiye aliyetoa vifaa hivi kwa ajili ya kurahisisha utekelezaji wa majukumu yenu ya kila siku,” amesema Mwalimu Busungu.
Aidha, ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita, Kipindi cha Pili, kwa kuwakumbuka walimu wenye mahitaji maalum, akisisitiza kuwa wao ni watumishi kama wengine, hivyo kuwapatia vifaa visaidizi kutawapa uhuru wa kufanya kazi kwa ufanisi na kujiona kuwa sehemu ya jamii wanayoihudumia.
Kwa upande wake, Afisa Elimu Maalum wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya, Bi. Hawa Mtonyole, amesema kuwa halmashauri hiyo ina walimu wanne wenye mahitaji maalum, ambapo walimu wawili tayari wamepatiwa vifaa visaidizi kulingana na mahitaji yao.
Amesema Mwalimu Edward Mwatimba amepatiwa kishikwambi, huku Mwalimu wa Shule ya Sekondari Bitimanya akipatiwa kompyuta mpakato.
Ameongeza kuwa Mwalimu wa Shule ya Sekondari Itewe atapatiwa kitimwendo ili kurahisisha utendaji wake, na mwalimu mwingine mwenye ulemavu wa ngozi naye atapatiwa kifaa stahiki.
“Mheshimiwa Rais amesisitiza kuwa walimu wote wenye mahitaji maalum watafikiwa kulingana na mahitaji yao, ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi,” amesema Bi. Mtonyole,
Naye Mwalimu Edward Mwatimba ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwakumbuka watu wenye mahitaji maalum na kuwapatia vifaa visaidizi vitakavyowarahisishia utendaji wa kazi zao za kila siku.
Kwa ujumla, Halmashauri ya Wilaya ya Chunya imeendelea kunufaika na juhudi za Serikali katika kipindi cha siku 100 za Mheshimiwa Rais, ambapo imepokea fedha, watumishi wapya kupitia ajira, pamoja na maboresho mbalimbali ikiwemo kuwafikia walimu wenye mahitaji maalum kwa kuwapatia vifaa visaidizi.
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254



Post a Comment