" DKT. NCHIMBI KUZINDUA JENGO LA VVIP KATIKA UWANJA WA NDEGE WA KIMATAIFA WA JULIUS NYERERE (JNIA)

DKT. NCHIMBI KUZINDUA JENGO LA VVIP KATIKA UWANJA WA NDEGE WA KIMATAIFA WA JULIUS NYERERE (JNIA)

Na Mwandishi wetu, Misalaba Media Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Emmanuel Nchimbi, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika hafla ya uzinduzi wa jengo jipya la Wageni Maarufu (VVIP) lililopo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) – Terminal ya Tatu, itakayofanyika Januari 16, 2026 jijini Dar es Salaam.‎Taarifa hiyo imetolewa leo Januari 15, 2025 na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Abubakar Kunenge, akimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert John Chalamila, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya uzinduzi huo.‎Mhe. Kunenge amesema jengo hilo limejengwa kwa viwango vya kisasa kwa lengo la kuboresha huduma za mapokezi kwa wageni waalikwa, viongozi wa kitaifa na kimataifa pamoja na watu mashuhuri wanaoingia na kutoka nchini kupitia uwanja huo.‎Aidha ameongeza kuwa uzinduzi wa jengo hilo ni sehemu ya jitihada za Serikali katika kuimarisha miundombinu ya usafiri wa anga na kuinua hadhi ya Tanzania kimataifa, hususan katika mapokezi ya wageni wakubwa.‎“Mradi huu ni maalum kwa ajili ya kuwahudumia wageni wakubwa wakiwemo viongozi wa ngazi mbalimbali na watu mashuhuri kutoka ndani na nje ya nchi,” amesema Mhe. Kunenge.‎Hata hivyo amesema kuwa ujenzi wa jengo la VVIP ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuboresha taswira ya Jiji la Dar es Salaam kama lango kuu la kuwakaribisha wageni wa ndani na nje ya nchi, sambamba na kuongeza ufanisi na viwango vya huduma katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere.‎Uzinduzi wa jengo hilo unatarajiwa kuongeza ubora wa huduma za usafiri wa anga, kuboresha uzoefu wa wageni na kuendelea kuiweka Tanzania katika ramani ya kimataifa kama nchi yenye miundombinu ya kisasa na huduma bora.

 

Post a Comment

Previous Post Next Post