
Na Mwandishi wetu, Misalaba Media
Taasisi ya Utambulisho wa Bidhaa Tanzania (GS1 Tanzania) imeadhimisha miaka 15 tangu kuanzishwa kwake, ikieleza mafanikio makubwa katika kuchochea ukuaji wa biashara, viwanda na kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya ndani na kimataifa.
Maadhimisho hayo yamefanyika leo, Januari 24, 2026 jijini Dar es Salaam, yakishirikisha wadau kutoka sekta binafsi, taasisi za umma pamoja na wataalamu wa teknolojia ya biashara.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa GS1 Tanzania, Fatma Kange, amesema taasisi hiyo imepitia safari ya mageuzi makubwa tangu kuanzishwa kwake, kutoka utekelezaji wa shughuli za kimsingi hadi matumizi ya mifumo ya kisasa inayotumia teknolojia za kidijitali.
Amesema GS1 Tanzania inaendelea kubadilika kulingana na mahitaji ya soko na kasi ya mabadiliko ya teknolojia, huku maandalizi ya maadhimisho makubwa ya kutimiza miaka 15 yakitarajiwa kufanyika rasmi Septemba mwaka huu.
“Kama taasisi tunajiuliza tulikotoka, tulipo na tunapoelekea. Teknolojia zinabadilika kwa kasi, na GS1 Tanzania ina wajibu wa kuhakikisha wanachama wake hawaachwi nyuma,” amesema Kange.
Ameongeza kuwa mageuzi hayo yanalenga kuwawezesha wazalishaji na wafanyabiashara kutambulisha bidhaa zao kwa ufanisi zaidi, kwa kuzingatia viwango vinavyokubalika kimataifa, hivyo kuongeza fursa za ushindani katika masoko mbalimbali.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Utafiti Viwanda wa TRIDO na Mwakilishi wa Mgeni Rasmi, Humfrey Ndosi, amesema GS1 Tanzania imekuwa chombo muhimu katika kusaidia viwanda vya ndani kuboresha ushindani wa bidhaa zao, hasa kupitia matumizi ya mifumo ya utambulisho inayotambulika kimataifa.
Ameeleza kuwa kabla ya kuanzishwa kwa GS1 Tanzania, wazalishaji wengi walikumbana na changamoto kubwa za kuingiza bidhaa zao sokoni, hali iliyosababisha baadhi yao kutegemea masoko ya nje.
Ndosi pia aliwasilisha salamu za wizara na kuipongeza GS1 Tanzania kwa mchango wake katika kukuza sekta binafsi, akibainisha kuwa serikali itaendelea kushirikiana na taasisi hiyo katika kujenga mazingira wezeshi ya biashara na kuimarisha miundombinu ya kiuchumi.
Amesema mafanikio ya GS1 Tanzania yametokana na ushirikiano mpana kati ya serikali na sekta binafsi, ukihusisha taasisi mbalimbali zikiwemo TRIDO, TBS, BRELA, SIDO, TPSF, ZNCC, TCCIA, CTI, TAHA, pamoja na vyama vya wazalishaji wa mazao na viungo.
Katika maadhimisho hayo, GS1 Tanzania pia imetangaza kuendeleza mageuzi ya kidijitali, yakiwemo maandalizi ya uzinduzi wa mfumo wa 2D Migration, unaolenga kuboresha zaidi utambulisho wa bidhaa za Tanzania na kuongeza ufanisi katika minyororo ya thamani ya biashara.
Ufunguzi wa maadhimisho hayo umetumika kutoa wito kwa Watanzania kujiamini, kujituma na kutumia fursa zilizopo katika mazingira bora ya biashara yanayoendelea kuwekwa na serikali.
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254



Post a Comment