Na Lydia Lugakila -Misalaba Media Mbeya Afisa Msimamizi wa Usimamizi wa Kodi, Bi. Jane Jisandu kutoka Mkoa wa Kodi Ilala, yupo mkoani Mbeya pamoja na timu yake kwa ajili ya kutoa mafunzo ya mfumo mpya wa ukusanyaji wa kodi za ndani ujulikanao kama IDRAS, kwa wafanyakazi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) pamoja na walipa kodi mkoani Mbeya.Akizungumza na Misalaba Media Januari 22, 2026, baada ya semina iliyoandaliwa na TRA Mkoa wa Mbeya kwa kushirikiana na Mowi Consulting, iliyofanyika katika ukumbi wa Beaco, Bi. Jisandu alisema mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi za kuimarisha ufanisi na uzingatiaji wa ulipaji kodi kupitia matumizi ya mifumo ya kidijitali. Semina hiyo iliwakutanisha wadau mbalimbali wa kodi wakiwemo wahasibu, wakaguzi wa hesabu na wafanyabiashara, ambapo walipatiwa elimu juu ya matumizi ya mfumo wa IDRAS na manufaa yake katika ukusanyaji wa kodi za ndani. Bi. Jisandu amesema timu hiyo itakuwa mkoani Mbeya kwa muda wa wiki mbili, ambapo wiki ya kwanza itaelekezwa katika kuwajengea uwezo wafanyakazi wa TRA kupitia mafunzo ya ndani (ToT – Training of Trainers), ili kuhakikisha wafanyakazi wote wanauelewa na kuutumia kikamilifu mfumo huo mpya. Ameeleza kuwa, baada ya hapo, mafunzo yataendelea kwa walipa kodi, ambapo wawakilishi wa wafanyakazi kutoka mikoa ya Mbeya, Rukwa na Songwe tayari wamekusanywa kwa ajili ya mafunzo hayo. Aidha,msimamizi huyo wa kodi amebainisha kuwa timu nyingine tayari zipo katika mikoa ya Iringa, Morogoro, Tabora, Mwanza, Arusha pamoja na Zanzibar, zikiendelea na zoezi la kuwajengea uwezo wafanyakazi wa ndani. Kwa mujibu wa Bi. Jisandu, wiki inayofuata imepangwa mahsusi kwa ajili ya wataalamu kusambaa katika mikoa mbalimbali, huku baadhi yao wakibaki Mbeya ili kuwafikia walipa kodi moja kwa moja, kuwasaidia wafanyakazi waliobaki ofisini, pamoja na kutoa elimu uso kwa uso.Ameongeza kuwa idadi ya wataalamu itaongezeka kutoka saba hadi kufikia 30 ili kuongeza nguvu na ufanisi wa utekelezaji wa mafunzo hayo. “Tutaendelea kufanya semina na kushiriki midahalo kupitia vyombo vya habari mbalimbali ikiwemo televisheni na redio, kwa lengo la kuwaandaa wadau katika mabadiliko haya na kuwaonesha namna bora ya kutumia mfumo huu ambao utapunguza changamoto na kuongeza ufanisi,” alisema Bi. Jisandu. Aidha, amesema mfumo wa IDRAS umeletwa katika kipindi ambacho makadirio ya kodi yanaendelea kufanyika, hivyo amewataka walipa kodi kujiandaa kuendana na mabadiliko hayo pindi mfumo utakapoanza kutumika rasmi. Amefafanua kuwa mamlaka hiyo inaondoka katika matumizi ya mifumo ya makaratasi na kuelekea katika mfumo wa kielektroniki, huku akisisitiza kuwa mafunzo hayo ni endelevu na yalianza rasmi mwezi Desemba, 2025 kupitia njia za masafa.🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254


Post a Comment