" KAMATI YA BUNGE TAMISEMI YAJENGEWA UWEZO KUPITIA MAFUNZO MAALUM

KAMATI YA BUNGE TAMISEMI YAJENGEWA UWEZO KUPITIA MAFUNZO MAALUM

Na Fabius Clavery, Misalaba Media.

‎Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Florent Kyombo, ameongoza kikao cha kamati hiyo wakati wa mafunzo maalum yaliyolenga kuwajengea uwezo wajumbe wa kamati katika utekelezaji wa majukumu yao ya kibunge.

‎Mafunzo hayo yalijikita katika kuelewa Muundo na Majukumu ya Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM–TAMISEMI), pamoja na sera na sheria mbalimbali zinazotekelezwa na ofisi hiyo katika kusimamia maendeleo na utoaji wa huduma kwa wananchi.

‎Akizungumza wakati wa kikao hicho, Mhe. Kyombo amesema mafunzo hayo ni muhimu katika kuiwezesha kamati kupata uelewa wa kina kuhusu mifumo ya utendaji wa TAMISEMI, hatua ambayo itaongeza ufanisi katika kazi za usimamizi, ushauri na ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi na programu za maendeleo katika ngazi za mikoa na mamlaka za serikali za mitaa.

‎Ameeleza kuwa kupitia mafunzo hayo, wajumbe wa kamati wataweza kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia misingi ya sera, sheria na miongozo iliyopo, hivyo kusaidia kuboresha uwajibikaji na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.

‎Mafunzo hayo ni sehemu ya jitihada za Serikali na Bunge katika kuhakikisha kamati za bunge zinaimarishwa kitaalamu ili ziweze kusimamia ipasavyo utekelezaji wa majukumu ya taasisi za umma chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI.


 


Post a Comment

Previous Post Next Post