" KIKAO CHA KAWAIDA CHA BARAZA LA WAZAZI CCM WILAYA YA MPANDA CHA KUFUNGA MWAKA 2025 CHAFANYIKA JANUARI 14, 2026

KIKAO CHA KAWAIDA CHA BARAZA LA WAZAZI CCM WILAYA YA MPANDA CHA KUFUNGA MWAKA 2025 CHAFANYIKA JANUARI 14, 2026

Baraza la Wazazi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Mpanda linafanya kikao chake cha kawaida cha kufunga mwaka 2025 tarehe 14 Januari 2026, kikao ambacho kinaongozwa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Mpanda, Ndugu Pius Buzumalle.

Katika kikao hicho, Ndugu Pius Buzumalle amewaomba wajumbe wa baraza kuwa na umoja na mshikamano wa dhati katika kuendeleza na kuimarisha Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Mpanda, huku akiwapongeza wajumbe kwa ushirikiano wao katika utekelezaji wa majukumu ya chama kwa mwaka mzima wa 2025 ambapo Mwenyekiti huyo ametumia nafasi hiyo kuwasalimia wajumbe na kuwatakia heri ya mwaka mpya 2026.

Akizungumzia Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, Baraza la Wazazi CCM Wilaya ya Mpanda linakipongeza Chama Cha Mapinduzi kwa ushindi mkubwa katika ngazi zote za uongozi ikiwemo Udiwani, Ubunge na Urais ambapo Jumuiya imeeleza kuridhishwa na matokeo hayo na kuishukuru CCM kwa kuendelea kushika dola.

Katibu wa Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Mpanda, Ndugu Jimotoli Jilala Maduka, ameeleza kuwa Jumuiya inaendelea kuwa imara na iko mstari wa mbele katika kutekeleza majukumu yake ya chama kwa ufanisi na weledi, akisisitiza umuhimu wa kila mjumbe kutimiza wajibu wake ndani ya Jumuiya na CCM kwa ujumla.

Ndugu Jimotoli ameendelea kuwasisitiza wajumbe kuimarisha umoja na mshikamano, pamoja na kushiriki kikamilifu katika kazi za Jumuiya ya Wazazi na Chama Cha Mapinduzi ili kuongeza ufanisi wa utendaji kazi kwa wanachama wote waliopo kwenye nafasi mbalimbali za chama. Katika hatua nyingine, Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Mpanda inatoa shukrani za dhati kwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mwenyekiti wa CCM Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuibuka mshindi wa kiti cha Urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2025, na kutamka wazi kuwa “Hongera sana”.

Kikao hicho pia kimejadili uimarishaji wa uhai wa Jumuiya ya Wazazi, ambapo Katibu wa Jumuiya amewahimiza wajumbe kuendelea kulipia ada za wanachama, kutoa hamasa ya uandikishaji wa wanachama wapya na kuendelea kutoa elimu katika ngazi za matawi, mashina na kata ili kuongeza idadi ya wanachama.

Katika ajenda ya elimu, Baraza limeelekeza nguvu katika Shule ya Sekondari na Ufundi Milala, iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda na kwamba Jumuiya imeendelea kuisemea na kuipambania shule hiyo kwa lengo la kuhakikisha eneo la shule linapangwa na kupimwa kwa wakati ili hatimaye shule ipate Hati Miliki ya Eneo la Shule.

Hatua hiyo imelenga kuweka mazingira rafiki ya kutafuta mwekezaji mzuri atakayesaidia kuendeleza mafunzo, sambamba na kurejesha hadhi ya shule hiyo ambayo awali ilikuwa ya mfano na bora kwa elimu ya sekondari na ufundi.

Aidha, Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Mpanda imeeleza kuridhishwa na mafanikio ya kisiasa yaliyopatikana katika Uchaguzi Mkuu wa 2025, ambapo jumla ya madiwani 13 na wabunge wawili (2) kutoka majimbo ya Mpanda Mjini na Nsimbo wanatokana na Jumuiya ya Wazazi.

Mafanikio hayo yametajwa kuwa matokeo ya umoja, mshikamano na hamasa kubwa iliyotolewa kwa wazazi kujitokeza kugombea nafasi za udiwani na ubunge.

Mwisho wa kikao, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Mpanda, Ndugu Pius Buzumalle, amelifunga rasmi baraza la kufunga mwaka 2025 kwa kuwashukuru wajumbe wote kwa kuunga mkono mipango na mikakati ya Jumuiya, hususan katika utekelezaji wa mradi wa shule na masuala mengine yaliyojadiliwa katika kikao hicho.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Mpanda, Ndugu Pius Buzumalle, akizungumza kwenye kikao.

Katibu wa Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Mpanda, Ndugu Jimotoli Jilala Maduka, akizungumza.




  

Post a Comment

Previous Post Next Post