" MADARAJA 5 YA DHARULA KAGERA KUKAMILIKA FEBRUARI 2026, WAKANDARASI WAZAWA WASHUKURU KUAMINIWA

MADARAJA 5 YA DHARULA KAGERA KUKAMILIKA FEBRUARI 2026, WAKANDARASI WAZAWA WASHUKURU KUAMINIWA

Na Fabius Clavery, Misalaba Media- Kagera

Ujenzi wa madaraja matano ya Dharula mkoani Kagera unaoendelea kutekelezwa kupitia Mradi wa SEQ unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Februari 2026, hatua itakayosaidia kuboresha mawasiliano ya barabara na kurahisisha shughuli za kijamii na kiuchumi kwa wananchi wa mkoa huo.

‎Akizungumza kuhusu utekelezaji wa miradi hiyo, Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Kagera, Mhandisi Samwel Joel Mwambungu, amesema ujenzi wa madaraja hayo ulianza rasmi mwezi Novemba mwaka 2024 kufuatia uharibifu mkubwa uliosababishwa na mvua za El Niño zilizoathiri miundombinu ya barabara kipindi hicho.

‎Mhandisi Mwambungu amebainisha kuwa madaraja yanayojengwa ni pamoja na Daraja la Kanoni  linalotekelezwa na mkandarasi Abemulo Contractors ndani ya Manispaa ya Bukoba, Daraja la Kamishango lililopo Wilaya ya Muleba linalotekelezwa na DRK Contractors ambalo limefikia asilimia 98 ya utekelezaji, pamoja na Daraja la Kyetema lenye asilimia 77 ya utekelezaji na Daraja la Kyanyabasa yanayotekelezwa na Gemen Engineering Constructors.

‎Aidha, Daraja la Karebe lenye urefu wa Dharula linatekelezwa na Milembe Constructors Ltd katika maeneo ya vijijini, ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia 73.

‎Kukamilika kwa miradi hiyo kunatarajiwa kuondoa changamoto za mawasiliano ya barabara zilizokuwa zikijitokeza nyakati za mvua, hali iliyokuwa ikiwalazimu wananchi kushindwa kupita au kusafirisha mazao na huduma muhimu.

‎Akizungumza kwa niaba ya wakandarasi wanaotekeleza miradi hiyo, Mkurugenzi wa Milembe Constructors Ltd, Oscar Byabato Ephraim, amesema wakandarasi wote wana dhamira ya kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati na kwa kuzingatia masharti ya mikataba waliyoingia na TANROADS.

‎Bw. Ephraim ameishukuru TANROADS pamoja na Wizara ya Ujenzi kwa kuendelea kuwaamini wakandarasi wa ndani na kuwapatia fursa ya kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati, ambayo awali ilikuwa ikitekelezwa zaidi na wakandarasi kutoka nje ya nchi.

‎Amesema hatua hiyo inaongeza uwezo, uzoefu na ushindani kwa wakandarasi wazawa katika sekta ya ujenzi nchini.

‎Madaraja hayo yanagharimu Zaidi ya shilingi Bilioni 45.








Post a Comment

Previous Post Next Post