WAKATI Taifa likiendelea na kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo, wananchi na viongozi wa mitaa katika Halmashauri ya Mji wa Kibaha mkoani Pwani, wametoa wito wa kuendelea kudumisha amani na utulivu, wakitaja mambo hayo kuwa ndiyo ngao pekee itakayolifanya Taifa liendelee kuwepo na kusonga mbele.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wadau hao wamebainisha kuwa bila amani hakuna shughuli yoyote ya kiuchumi inayoweza kufanyika, huku wakisisitiza kuwa mshikamano wa Watanzania unapaswa kukumbatiwa na kila mwananchi.
Mfanyabiashara wa Soko la Uyaoni lililopo Maili Moja, Cletus Kasanga, amesema kuwa kipaumbele cha kila Mtanzania kinapaswa kuwa ni kuiombea nchi iendelee kuwa na utulivu. Amewatahadharisha vijana kuwa makini na watu wenye nia mbaya wanaowaza na kupanga kuvuruga amani ya nchi kwa maslahi yao binafsi.
"Wote tunaiombea nchi yetu iendelee kuwepo na tusiruhusu itoweke kwani bila amani hatuwezi kufanya lolote. Sisi tunahamasisha amani na tunataka tuendelee kudumisha utulivu kwani ni ngao za nchi yetu. Vijana wamche Mungu ili atulinde na wabaya wanaotaka kutuharibia nchi yetu," alisema Kasanga.
Naye Isaya Lwinga, ambaye pia ni mfanyabiashara katika soko hilo, amewataka vijana kutokubali kutumiwa kama daraja la kuvunja amani, akibainisha kuwa nguvu walizonazo zinapaswa kuelekezwa katika kulinda usalama wa nchi na kufanya kazi za uzalishaji.
"Amani yetu ndiyo silaha yetu na ndiyo usalama wetu. Sisi vijana ndiyo wa kuilinda kwani bado tuna nguvu na ndiyo watu wanatutumia; tusikubali kuivunja. Utulivu unatusaidia tufanye shughuli zetu bila shida yoyote na mshikamano unahitajika kila wakati," alisisitiza Lwinga.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa wa Simbani, Nasra Madenge, amewataka wananchi kuwa na uvumilivu na kuendelea kuwasikiliza viongozi wao ili kudumisha jadi ya utulivu ambayo Tanzania imekuwa ikisifika kwayo kwa miongo mingi.
"Tunataka amani yetu iendelee kuwepo kwani hiyo ni jadi yetu; hatujazoea uvunjifu wa amani. Kikubwa ni wananchi kuwa na uvumilivu na wawe watulivu kwani hayo ndiyo maisha yetu. Tuendelee kuwasikiliza viongozi wetu kwani bila ya mshikamano hakuna kitakachoweza kufanyika na kuleta maendeleo," alisema Mwenyekiti huyo.
Kauli hizi za wakazi wa Kibaha zinakuja wakati ambapo Serikali inaendelea kusisitiza umuhimu wa utulivu wa ndani kama nyenzo ya kuvutia wawekezaji na kutekeleza Dira ya Maendeleo ya 2050, huku mshikamano wa kitaifa ukitajwa kama msingi mkuu wa mafanikio yote ya kijamii na kiuchumi.
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254
Post a Comment