UKUMBI wa kihistoria wa Nkurumah katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Januari 12, 2026, umekuwa chimbuko la darasa huru la uzalendo na ukomavu wa kifikra, wakati wa mdahalo wa kumbukizi ya Miaka 62 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
Mdahalo huo umeibua hoja nzito kuhusu umuhimu wa vijana kuwa na ujasiri (confidence) wa kuhoji na kukosoa, lakini wakifanya hivyo kwa kutumia nguvu ya hoja badala ya matusi na kejeli.
Katika mdahalo huo uliobeba taswira ya ushiriki wa vijana katika maendeleo, ujumbe mkuu uliotawala ni kuwa hoja hujibiwa kwa hoja, na majibu ya hoja njema siku zote ni maafikiano yanayochochea maendeleo ya Taifa.
Kukosoa kwa Mashiko, si kwa Mihemko
Makamu wa Rais wa Serikali ya Wanafunzi (DARUSO), Joyce Semkuyu, amekuwa kivutio kikubwa katika mdahalo huo kwa kusisitiza kuwa vijana hawatakiwi kuwa "ndio mzee" kwa kila jambo. Alibainisha kuwa ili Taifa lisonge mbele, vijana lazima wawe na ujasiri wa kukosoa pale panapostahili, lakini akatoa angalizo la msingi kuhusu namna ya kufanya ukosoaji huo.
"Ili kuhakikisha taifa letu linasonga mbele, vijana hatutakiwi kukubali kila kitu. Tunapaswa kukosoa pale panapostahili, lakini tufanye hivyo kwa hoja zenye mashiko. Uzalendo ni kuwa mbele katika shughuli za kitaifa huku tukiilinda amani yetu," alisema Semkuyu, huku akishangiliwa na mamia ya wanachuo.
Kauli hiyo imetafsiriwa kama mwongozo kwa vijana wanaotumia mitandao ya kijamii, ambapo mara nyingi mijadala imekuwa ikipoteza mwelekeo kwa kutawaliwa na matusi na chuki badala ya maarifa.
Mitandao ya Kijamii: Jukwaa la Hoja, si Vurugu
Wadau wengine waliochangia katika mdahalo huo wamewatahadharisha vijana dhidi ya mtego wa kutumia teknolojia kubomoa nchi. Nathanael Maseke, mkazi wa Dar es Salaam, alisisitiza kuwa njia nzuri ya kuwasilisha malalamiko ni kupitia taratibu rasmi na zenye staha, na si kwa kutumia vurugu au upotoshaji mtandaoni.
"Tunapaswa kuepuka kutumia mitandao kupotosha au kueneza chuki. Kijana mwenye ujasiri na anayejiamini hahitaji kutukana ili asikike; anahitaji kupangilia hoja yake vizuri ili serikali na jamii iweze kumwelewa na kufanya naye kazi," alisema Maseke.
Kwa upande wake, Saud Abdallah amewahimiza vijana kuiamini serikali yao kutokana na maendeleo makubwa yaliyofanyika katika sekta za afya na elimu, akisisitiza kuwa kulinda amani na utulivu ni sehemu ya utamaduni wa Mtanzania ambao haupaswi kuchafuliwa na vurugu za kisiasa.
Mdahalo huo umebainisha kuwa kijana anayejiamini ni yule anayeweza kusimama katika majukwaa makubwa kama Nkurumah na kuwasilisha wazo mbadala bila kuogopa, lakini kwa lugha ya staha. Hali hii inaendana na falsafa ya "Hoja hujibiwa kwa Hoja," ambapo maafikiano yanayopatikana ndiyo yanayofungua milango ya miradi mikubwa nchini.
Hii ndiyo Tanzania inayojengwa; nchi ambayo msomi na kijana wa mtaani wanaunganishwa na lugha ya kistaarabu. Ujumbe wa mdahalo wa leo ni wazi kwa vijana: "Jiamini, hoji, kosoa kwa heshima, na tanguliza maslahi ya Taifa mbele ya matusi."
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254


Post a Comment