Mafanikio makubwa ya timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars ,katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika 2025 yameendelea kuibua mjadala mzito miongoni mwa mashabiki wa soka katika ukanda wa Afrika Mashariki na kwingineko.
Wakati Tanzania ikisherehekea hatua hiyo kubwa wapo baadhi ya watu na majirani wanaoonekana kuteseka na kusononeka kutokana na mafanikio hayo ambayo kwa uhakika si ya bahati mbaya bali ni matunda ya uwekezaji mkubwa uliofanywa katika miundombinu ya michezo na usimamizi wa michezo ikiwamo soka.
Ni vyema wanaobeza wakaelewa kuwa mafanikio ya Taifa Stars ni matokeo ya amani ya kudumu iliyopo nchini Tanzania ambayo imetoa fursa ya kuendeleza vipaji vya vijana na kuifanya ligi kuu ya Tanzania kuwa miongoni mwa ligi bora na zenye mvuto mkubwa barani Afrika jambo linalozalisha wachezaji makini na wenye ushindani wa hali ya juu.
Kabla ya michuano hii kuanza baadhi ya majirani waliibeza Taifa Stars wakiamini ingeondolewa mapema katika hatua za awali na hata baada ya timu hiyo kufuzu hatua ya kumi na sita bora bado kejeli zimeendelea mitandaoni zikidai kuwa imefuzu bila kushinda mechi yoyote jambo ambalo ni tafsiri ya wivu wa mafanikio.
Hata hivyo, kufuzu kwa Taifa Stars kumeibua tafakuri mpya miongoni mwa wachambuzi wa kimataifa ambao wanakiri kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa kutokana na ligi yake ya ndani kuwa imara na kutoa idadi kubwa ya wachezaji wanaocheza michuano hiyo mikubwa.
Wachambuzi kutoka nchi jirani kama Kenya wameanza kukiri hadharani kuwa wakati Tanzania ikifuzu AFCON mara kwa mara tangu 2019 hadi 2025 kwa misingi ya ushindani wao wamebaki wakitegemea bahati ya uenyeji au kutoa visingizio huku wakishindwa kuwekeza kama ilivyofanya Tanzania.
Mafanikio ya soka nchini Tanzania yanajidhihirisha kupitia maendeleo ya klabu za ndani kimataifa na mifumo ya kukuza vipaji vya vijana ambayo imeifanya Taifa Stars kuwa timu iliyokomaa yenye mwelekeo sahihi na mustakabali mzuri.
Kuteseka kwa majirani na baadhi ya watu mitandaoni ni ishara kuwa Tanzania imekuwa mfano wa kuigwa na somo kubwa kwa ukanda huu kuwa hakuna mkato katika soka la kisasa bali uwekezaji wa muda mrefu, mipango thabiti na usimamizi bora ndiyo njia pekee ya kupata mafanikio endelevu.
Badala ya kutoa kauli za kubeza na kukejeli ni vyema wadau wa soka wakajifunza kutoka Tanzania jinsi ya kutumia amani na rasilimali zilizopo kuinua kiwango cha mchezo huo na kuacha tabia ya kupuuza hatua kubwa zinazopigwa na taifa hili.
Ujumbe kwa wale wanaoposti maoni ya dhihaka na lugha zisizofaa mitandaoni ni kwamba chuki haitawasaidia kupata mafanikio bali kuelewa kuwa michezo ni sayansi na Tanzania imeshafanya ugunduzi wa dawa ya ushindi kupitia umoja na uwekezaji.
Jamii inapaswa kupuuza jumbe hizo za kejeli za uchochezi na badala yake iendelee kuishangilia Taifa Stars ambayo kwa sasa ni kielelezo cha ukomavu wa soka la Afrika Mashariki huku ikiendelea kuchanua katika hatua za mtoano. Hakika kila tone la jasho la wachezaji wa kitanzania uwanjani ni kielelezo cha amani tuliyonayo na dhamira ya dhati ya serikali na wadau wa soka kuhakikisha bendera ya Tanzania inapepea juu kileleni mwa mafanikio ya soka barani Afrika na duniani kwa ujumla.
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

Post a Comment