Na Fabius Clavery, Misalaba Media -Kagera
Mbunge wa Jimbo la Muleba Kaskazini, Mhe. Adonis Alfred Bitegeko, jana tarehe 5 Januari 2025, ametembelea Kituo cha Afya Izigo kilichopo Kata ya Izigo, Wilaya ya Muleba , ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kujionea hali ya utoaji wa huduma za afya katika jimbo lake.
Katika ziara hiyo, Mbunge ametembelea kukagua majengo, miundombinu na vifaa tiba, ambapo Mhe. Bitegeko amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na Serikali kwa kuendelea kukiimarisha kituo hicho kwa viwango bora na vya kisasa, hatua inayochangia kuboresha huduma za afya kwa wananchi wa Kata ya Izigo na maeneo ya jirani.
Aidha, Mhe. Bitegeko amefanya mazungumzo na uongozi wa kituo hicho ukiongozwa na Mganga Mfawidhi, Dkt. Attackson Laurent Mwambeso, ambapo wamejadili kwa kina hali ya utoaji wa huduma, mafanikio yaliyopatikana pamoja na changamoto zinazokikabili kituo hicho.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Dkt. Mwambeso amemueleza Mbunge kuwa miongoni mwa changamoto kubwa ni chumba cha upasuaji kutofanya kazi kutokana na kukosekana kwa umeme wa uhakika, pamoja na Idara ya Meno kushindwa kutoa huduma kutokana na ukosefu wa mtaalamu wa afya ya kinywa. Ameongeza kuwa kituo hicho bado kinahitaji wataalamu zaidi ili kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Kwa upande wake, Mhe. Bitegeko ameahidi kukipambania kituo hicho ili changamoto hizo zipatiwe ufumbuzi wa haraka, akisisitiza kuwa sekta ya afya ni kipaumbele chake, kutokana na uzoefu wake wa awali alipokuwa mtumishi wa Serikali katika Wizara ya Afya kabla ya kuchaguliwa kuwa Mbunge.
Baada ya kukagua miundombinu na huduma zinazotolewa katika kituo hicho, Mhe. Bitegeko ametoa vifaa mbalimbali ikiwa ni pamoja na mashuka 19 na blanketi 19 kwa ajili ya wagonjwa, pamoja na sare maalum 10 za upasuaji (operating suites) zitakazotumiwa na madaktari na wauguzi, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali za kuboresha mazingira ya utoaji wa huduma za afya.
Uongozi wa kituo hicho pamoja na wananchi wa Izigo, wameeleza matumaini yao kuwa jitihada na ufuatiliaji wa Mbunge zitaendelea kuwa chachu ya maboresho ya huduma za afya katika Jimbo la Muleba Kaskazini.
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254





Post a Comment