Katika kile kinachoonekana kuwa ni mwendelezo wa juhudi za kulinda utulivu na mshikamano wa kitaifa mchambuzi mashuhuri wa masuala ya kisiasa na teknolojia nchini anayejulikana kama Djsma255 ameelezea kusikitishwa kwake na mienendo ya baadhi ya watumiaji wa mitandao ya kijamii wanaotumia vibaya uhuru huo kuchafua imani za dini.
Msisitizo huo umekuja kufuatia kusambaa kwa video za mwanamitandao Clemence Mwandambo ambaye ni mkazi wa mkoa wa Mbeya yenye maudhui yenye kukashfu imani za dini tofauti zikiwemo za Kikristo na Kiislamu jambo ambalo ni hatari kwa usalama na umoja wa nchi.
Djsma255 amebainisha kuwa uhuru wa mitandao unatumika vibaya na kwamba na baadhi ya watu wakibomoa misingi ya heshima na staha kwa kutoa kauli za dharau dhidi ya Mwenyezi Mungu na Mitume Wake jambo ambalo haliwezi kukubalika katika jamii yoyote iliyostaarabika.
Mchambuzi huyo amefafanua kuwa vitendo hivyo vya kejeli dhidi ya imani za kidini ni jambo zito na la hatari zaidi kuliko mijadala mingine yoyote kwani linagusa hisia za ndani za binadamu na linaweza kusababisha mpasuko mkubwa wa kijamii ikiwa hakutakuwa na hatua madhubuti za kukemea.
Amesema kuwa ameshangazwa na ukimya wa baadhi ya viongozi na wadau ambao wamekuwa wepesi kukemea masuala mengine lakini wameacha jambo hili la kashfa dhidi ya Mwenyezi Mungu likiendelea kuchafua hali ya hewa mitandaoni. Kwa mujibu wa Djsma255 matumizi hayo ya teknolojia yanapaswa kuwa chombo cha kuelimisha na kuunganisha jamii na sio kuwa uwanja wa kutupa cheche za kashfa zinazoweza kuwasha moto wa kidini ambao ni vigumu kuuzima pindi unapoanza.
Hadi sasa Clemence Mwandambo anaripotiwa kuwa chini ya vyombo vya kisheria akikabiliwa na tuhuma za kukashifu imani za dini baada ya kujijengea umaarufu usio na tija kwa kuzungumza kauli zinazovuka mipaka ya kisheria na kimaadili.
Maoni mbalimbali kutoka kwa wananchi mitandaoni yameonyesha hisia tofauti huku wengi wakilaani vikali vitendo hivyo na kuitaka serikali kuchukua hatua kali za kisheria ili iwe fundisho kwa wengine wanaodhani uhuru wa kutoa maoni ni tiketi ya kutukana na kudhalilisha imani za wengine. Baadhi ya wananchi wameeleza kuwa mchezo wa kuchezea imani za dini ni mauti na haupaswi kupewa nafasi wala kutafutiwa utetezi wa aina yoyote kwani dini ndiyo mhimili wa maadili ya watanzania wengi.
Pamoja na malalamiko hayo kuna sauti zinazosisitiza umuhimu wa kumpuuza mhusika huyo kwa kumtaja kuwa huenda hana utimamu wa akili huku wengine wakiionya jamii kutozidi kusambaza video hizo kwani kufanya hivyo ni kumpa nafasi zaidi ya kueneza upuuzi na chuki.
Serikali kupitia vyombo vyake vya usalama imekuwa ikisisitiza kuwa Tanzania ni nchi isiyo na dini rasmi lakini inaheshimu na kulinda uhuru wa kila mwananchi kufuata imani yake bila kuingiliwa wala kudhihakiwa. Kwa muktadha huo hatua ya kumshikilia mhusika huyo ni uthibitisho kuwa mamlaka zipo macho kuhakikisha kuwa amani iliyopo haichezewi na mtu yeyote kwa kisingizio cha uhuru wa habari au usemi.
Ni dhahiri kuwa taifa hili linahitaji amani na mshikamano ili kusonga mbele kimaendeleo na sio mizozo ya kidini wala kisiasa inayoweza kurudisha nyuma juhudi za kujenga nchi.
Ujumbe wa mchambuzi Djsma255 umekuja kama tahadhari muhimu kwa vijana na watumiaji wote wa mitandao ya kijamii kuelewa kuwa kuna mipaka kati ya kutoa maoni na kufanya uhalifu wa kashfa.
Hakika maisha ya mwanadamu na utambulisho wake wa kiroho ni vitu vitakatifu vinavyopaswa kuheshimiwa na kila mmoja wetu ili kudumisha heshima ya Tanzania kama kisiwa cha amani na utulivu katika ukanda wa Afrika Mashariki na dunia kwa ujumla.
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254
Post a Comment