" MRADI WA MAJI UPO HATARINI KUKWAMA, NAIBU WAZIRI AKWAZIKA NA KASI YA UTEKELEZAJI: WANATAKA TUAMINI MANENO YAO TU

MRADI WA MAJI UPO HATARINI KUKWAMA, NAIBU WAZIRI AKWAZIKA NA KASI YA UTEKELEZAJI: WANATAKA TUAMINI MANENO YAO TU


Na Fabius Clavery, Misalaba Media-Kagera.

Licha ya mkataba wa utekelezaji wa Mradi wa Maji wa Rwakajunju, unaotekelezwa chini ya Mradi wa Miji 28 Kayanga wilayani Karagwe, kutarajiwa kukamilika ifikapo Desemba 2025, hadi kufikia Januari 16, 2026 utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 70 pekee.

‎Akizungumza wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi huo, Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo Mathew, ameonesha kutoridhishwa na kasi ndogo ya utekelezaji, hali iliyomlazimu kutoa maelekezo mazito kwa mkandarasi anayetekeleza mradi huo, kampuni ya Afcons Infrastructure Limited pamoja na mkandari mshauri kampuni ya WAPCOS Limited

‎Mhandisi Kundo amemtaka mkandarasi huyo kuhakikisha anakamilisha mradi kwa wakati baada ya Serikali kumuongezea muda wa utekelezaji wa miezi tisa, akisisitiza kuwa hakuna sababu ya kuendelea kushuhudia ucheleweshaji katika hatua muhimu za mradi.

‎Aidha, Naibu Waziri amemuelekeza mkandarasi mshauri kuongeza weledi, umakini na uwajibikaji katika kusimamia utekelezaji wa mradi huo, akieleza kuwa hadi sasa anaonekana kuwa na changamoto katika kumdhibiti na kumsimamia ipasavyo mkandarasi mkuu.

‎Amefafanua kuwa licha ya mradi kufikia asilimia 70 kwa ujumla, maeneo muhimu ndiyo yaliyo nyuma zaidi katika utekelezaji, hali aliyosema haikubaliki na inawachukiza wananchi. Kwa mujibu wa Naibu Waziri, ujenzi wa mitambo ya kutibu na kuchuja maji umefikia asilimia 45 pekee, huku eneo la kuchotea maji (Intake/Kichoteo) likiwa limefikia asilimia 32.

‎“Wanataka tuwaamini kwa maneno yao kila siku, papapa booo… hatutakubali. Haya mambo tumeenda nayo kwa zaidi ya miaka miwili sasa, na bado tumeamua kuwaongezea muda wa miezi tisa. Safari hii hatutaki ahadi, tunataka kuona kazi halisi ikikamilika kwa wakati. Haya maji hayawezi kutoka bila pampu, hayawezi kutoka bila transfoma, na hayawezi kutoka bila kutibiwa. Hivi ndivyo vitu tunataka kuviona" amesema Naibu waziri Kundo.

‎Vilevile, Mhandisi Kundo amesema kuwa hadi sasa mitambo ya kusukuma maji (pampu) pamoja na mitambo ya umeme bado haijafika eneo la mradi, jambo linaloashiria uwezekano wa kuendelea kuchelewesha kukamilika kwa mradi huo endapo hatua za haraka hazitachukuliwa.

‎Serikali imeeleza kuwa itaendelea kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa mradi huo ili kuhakikisha wananchi wa Wilaya ya Karagwe na maeneo yote yanayolengwa wanapata huduma ya maji safi na salama kwa wakati uliopangwa.

‎Awali, akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Mhandisi Magreth Nyange, Msimamizi wa Mradi kutoka Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Bukoba (BUWASA), amesema mradi huo unatarajiwa kuhudumia wananchi takribani 352,790 kutoka vijiji 34 vilivyopo ndani ya kata 12.

‎Mradi wa Maji wa Rwakajunju unatarajiwa kugharimu jumla ya Shilingi bilioni 64 za Kitanzania hadi kukamilika kwake ukiwa unatekelezwa na Kampuni ya .













Post a Comment

Previous Post Next Post