" MWAKIBINGA ASIFU MSIMAMO WA RAIS SAMIA KATIKA KULINDA HAKI NA UTAWALA WA SHERIA

MWAKIBINGA ASIFU MSIMAMO WA RAIS SAMIA KATIKA KULINDA HAKI NA UTAWALA WA SHERIA


Na Mwandishi wetu, Misalaba Media

‎Mchambuzi wa masuala ya kisiasa, Philipo Mwakibinga, ameisifu hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, akisema imeweka mwelekeo sahihi wa kuimarisha haki, uwajibikaji na maendeleo ya Taifa.

‎Akizungumza na waandishi wa habari leo 14 January 2026 Jijini Dar es salaam kufuatia Hotuba ya Rais kwenye Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Majaji na Mahakimu uliofanyika Januari 13, 2026 jijini Dodoma, Mwakibinga amesema hotuba hiyo imegusa kwa kina masuala nyeti yanayohusu mfumo wa utoaji haki hapa nchini.

‎Kwa mujibu wa Mwakibinga, Rais Samia amedhihirisha dhamira ya dhati ya Serikali katika kulinda uhuru wa Mahakama, kuimarisha utawala wa sheria na kuhakikisha wananchi wanapata haki kwa wakati na kwa usawa.

‎“Rais ameonyesha wazi kuwa hakuna maendeleo ya Taifa bila haki. Ameweka msisitizo mkubwa juu ya uwajibikaji wa taasisi za haki na wajibu wa kila mhimili wa dola kutekeleza majukumu yake kwa uadilifu,” alisema Mwakibinga.

‎Aidha ameongeza kuwa kauli za Rais zinatoa ujumbe mzito kwa watendaji wa sekta ya sheria, akiwemo Mahakama, Baraza la Mawaziri na Bunge, kuhakikisha wanaheshimu mipaka ya kikatiba na kushirikiana kwa lengo la kuhudumia wananchi.

‎Mwakibinga pia amebainisha kuwa hotuba hiyo ni mwendelezo wa juhudi za Rais Samia za kujenga Taifa linalozingatia misingi ya haki, amani na mshikamano wa kitaifa, akisisitiza kuwa bila mfumo imara wa haki, maendeleo hayawezi kupatikana.

‎Kwa ujumla, amesema hotuba ya Rais kwenye mkutano huo ni dira muhimu kwa mustakabali wa sekta ya sheria nchini na kielelezo cha uongozi unaotambua mchango wa Mahakama katika ustawi wa Taifa.

Post a Comment

Previous Post Next Post