Na Mwandishi wetu, Misalaba Media
Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rishwa (TAKUKURU) imekamilisha operesheni ya kuwakamata raia wawili wa China waliokuwa wakitafutwa kwa tuhuma za utakatishaji fedha na ufunguaji wa makampuni hewa.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mkuu wa TAKUKURU,Kinondoni Christian Nyakizee amesema kuwa operesheni hiyo ilifanyika Januari 5, 2026, na iliwakuta watuhumiwa Yao Licong na Wang Weisi, wakazi wa Oysterbay Phonex Apartments, Kinondoni, wakiwa na kiasi kikubwa cha fedha.
“Watuhumiwa hawa walikamatwa wakiwa na dola za Kimarekani 707,075 (sawa na Shilingi 1,732,333,750) pamoja na Shilingi za Kitanzania 281,450,000, zilizokutwa ndani ya gari lao,” amesema Nyakizee.
Pia ameongeza kuwa fedha hizo zinashukiwa kuwa ni matokeo ya utakatishaji wa fedha kupitia taarifa za kadi za benki zilizoibiwa kutoka kwa watu mbalimbali nje ya nchi.
"Watuhumiwa hao wameshindwa kuthibitisha uhalali wa fedha walizokamatwa nazo kwani hawana biashara halali au stakabadhi zinazothibitisha upatikanaji wa fedha hizo na niwahakikishie tu ukamataji huu ulifanyika mbele ya Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Oysterbay, ambaye alithibitisha uwepo wa kiasi hicho cha fedha"ameeleza Nyakizee
Mkuu wa TAKUKURU pia amebainisha kuwa Yao Licong alikuwa akitafutwa kwa tuhuma za ufunguaji wa makampuni hewa matano yanayochunguzwa kwa makosa ya ukwepaji kodi na utakatishaji fedha kiasi cha Shilingi Trilioni 1.8, ambayo haikutozwa kodi kwa kipindi cha 2019 hadi 2025.
Watuhumiwa hawa tayari wamefikishwa mahakamani na kesi yao ya awali imefunguliwa katika Mahakama ya Kisutu, shauri la uhujumu uchumi.
“TAKUKURU imetoa tahadhari kwa Watanzania wote wenye tamaa ya kutaka kupata utajiri haraka kwa njia zisizo halali, kuacha mara moja kufungua makampuni hewa au kushirikiana na raia wa kigeni kwa lengo la kutumia taarifa za kadi zilizoporwa,” ameongeza Nyakizee.
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

Post a Comment