
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Carolyne Nombo, akizungumza wakati wa ufunguzi wa warsha ya kujenga uelewa kwa wadau wa elimu kuhusu mkakati na miongozo ya kitaifa ya matumizi ya teknolojia za kidijitali katika sekta ya elimu, iliyofanyika Januari 14, 2026 jijini Dodoma.
Na Meleka Kulwa –, Dodoma
Serikali kupitia Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia imesema matumizi ya teknolojia za kidijitali katika elimu ni muhimu kwa maendeleo ya Taifa na maandalizi ya rasilimali watu wenye ujuzi unaoendana na mabadiliko ya teknolojia na soko la ajira Duniani.
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Carolyne Nombo, Januari 14, 2026, Jijini Dodoma, wakati akifungua warsha ya kujenga uelewa kwa wadau wa elimu kuhusu mkakati na miongozo ya Kitaifa ya teknolojia za kidijitali.
Profesa Nombo amesema kuwa mabadiliko ya kidijitali si chaguo bali ni hitaji la lazima, akibainisha kuwa dira ya taifa inategemea uwepo wa nguvukazi yenye ujuzi wa kidijitali, ubunifu na uwezo wa kuendana na mabadiliko ya teknolojia.
Amesema Serikali imewekeza kununua vifaa vya TEHAMA katika shule za msingi, sekondari, vyuo vya ualimu, taasisi za TVET na vyuo vikuu, pamoja na kujenga maabara za kompyuta, huku jitihada za kuunganisha wilaya zote na taasisi za elimu kuimarisha matumizi ya intaneti zikishughulikiwa.
Profesa Nombo amebainisha pia kuwa Serikali imeanzisha programu za kimkakati, ikiwemo Samia Scholarship, inayofadhili vijana wa Kitanzania kusomea Sayansi ya Takwimu, Akili Bandia na Roboti katika vyuo vya kimataifa, ili kurejea wakiwa na ujuzi wa kimataifa unaosaidia kuendeleza teknolojia za kisasa.
Aidha, amesema kuwa Wizara imeandaa Mkakati wa Taifa wa Elimu ya Kidijitali na miongozo yake ili kuweka mfumo wa kitaifa wa kuratibu mageuzi ya kidijitali katika ngazi zote za elimu, zikiwemo elimu rasmi na isiyo rasmi. Mkakati huo unaweka mkazo katika utekelezaji kwa vitendo kwa taasisi zote za elimu, ikilenga kuboresha ufundishaji, ujifunzaji, tathmini na usimamizi wa elimu.
Pia, amesema kuwa Utekelezaji wa mkakati unapaswa kuanza kwa kuimarisha misingi ya kidijitali ikiwemo upatikanaji wa intaneti, miundombinu ya TEHAMA, vyanzo vya umeme vya kuaminika, pamoja na matumizi ya majukwaa ya kujifunzia mtandaoni yaliyoidhinishwa.
Aidha, amebainisha kuwa Taasisi za elimu zinapaswa kuendeleza ujifunzaji mseto na wa mtandaoni, huku zikihakikisha usawa na ujumuishaji kwa wanafunzi wa vijijini, wenye ulemavu na walioko katika mazingira magumu.
Profesa Nombo amesema kuwa walimu ni nguzo kuu ya mageuzi ya kidijitali, akisisitiza kuwa teknolojia haiwezi kuchukua nafasi ya mwalimu bali inalenga kuongeza ufanisi na ubunifu katika ufundishaji na ujifunzaji. Vyuo vya ualimu, vyuo vikuu na taasisi zote za mafunzo zinapaswa kujumuisha ufundishaji wa kidijitali, ujumuishaji wa TEHAMA, uelewa wa akili bandia na stadi za sayansi ya takwimu katika mafunzo.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuzingatia maadili, ulinzi wa data na uadilifu wa kitaaluma katika matumizi ya teknolojia za kidijitali. Utekelezaji wa sheria ya ulinzi wa data ni msingi katika sekta ya elimu.
Aidha, amesema kuwa Ufanisi wa mkakati wa elimu ya kidijitali unahitaji ushirikiano wa karibu kati ya Serikali, taasisi za udhibiti, sekta binafsi na washirika wa maendeleo.
Awali akizungumza,Naibu Katibu Mkuu wa Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Daniel Mushi, amesema kuwa warsha hiyo ni muhimu kwa kujenga uelewa wa pamoja miongoni mwa wadau, kuboresha ufundishaji, ujifunzaji, na kukuza ubunifu miongoni mwa walimu na wanafunzi.
Hata hivyo, amesema kuwa Warsha hiyo itazingatia nyaraka muhimu za kitaifa, ikiwemo miongozo na mkakati wa teknolojia za kidijitali, huku maandalizi yakiimarisha utekelezaji wa malengo kwa ufanisi.
Warsha hiyo ya siku mbili, inayofanyika Januari 14–15, 2026, inawakutanisha wataalam na viongozi mbalimbali wakiwemo makatibu wakuu, wakuu wa vyuo vikuu, viongozi wa VETA, wakuu wa vyuo vya ualimu, taasisi za maendeleo pamoja na wadau wengine wa elimu kutoka sekta za umma na binafsi.










🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254
Post a Comment