" Simba SC Yazindua Kampeni ya Ushindi Dhidi ya Esperance

Simba SC Yazindua Kampeni ya Ushindi Dhidi ya Esperance

 

Semaji Ahmed Ally, kiongozi wa Simba Sports Club, amewahimiza Wanasimba kuacha lawama na migawanyiko, na kuungana kama “Nguvu Moja” kuelekea mchezo muhimu wa Jumapili dhidi ya Esperance ya Tunisia.

Akizungumza na Wanasimba kutoka Tawi la Wekundu wa Kurasini Mji Mpya, Semaji alisema kuwa mashabiki ndio nguzo ya msingi ya timu, na ndio sababu kiingilio kwa mechi hiyo kimepunguzwa ili kila Mwanasimba aweze kuhudhuria uwanjani.

“Mzunguko tumewawekea Tsh 3,000, VIP C ni Tsh 5,000, VIP B ni Tsh 10,000, VIP A ni Tsh 20,000, na Platinum tumeshusha kutoka Tsh 150,000 hadi Tsh 100,000. Tanzanite ni Tsh 150,000 pekee, na tiketi tayari zimeshakwisha kusafirishwa,” alisema Semaji.

Semaji alisisitiza kuwa Simba ina uwezo wa kufanya maajabu, akibainisha kuwa timu inahitaji shauku na ushirikiano wa mashabiki kuibuka na ushindi.

“Tarehe moja tunakwenda kufikia Benjamin Mkapa Stadium, pamoja na hoja kwamba ni pabaya, tunakwenda kuasha matumaini. Tunakwenda kuandika historia mpya Afrika. Tumebakiwa na alama tisa pekee, tunaanza nazo na Esperance,” alisema Semaji.

Aidha, aliwashauri Wanasimba kushirikiana na kuacha kulaumiana, na kuhakikisha kila mmoja anachangia katika juhudi za timu kufika robo fainali.

“Huu sio muda wa kulaumiana, huu ni muda wa kuangalia tunashindaje mechi tatu zijazo. Hii ni safari ya kuishangaza Afrika,” aliongeza Semaji.

Semaji aliweka msisitizo kuwa ushindi si jukumu la wachezaji peke yao bali ushirikiano kati ya timu na mashabiki ndio utakaoamua hatima ya Simba SC katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Post a Comment

Previous Post Next Post