Na Lydia Lugakila - Misalaba mediaMbeyaMamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Mbeya, kwa kushirikiana na Mowi Consulting, imeendesha semina maalum kwa wadau wa kodi wakiwemo wahasibu, wakaguzi wa hesabu na wafanyabiashara, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha ufanisi na uzingatiaji wa ulipaji kodi kupitia matumizi ya mifumo ya kidijitali.Semina hiyo imefanyika Januari 22, 2026 katika Ukumbi wa Beaco, jijini Mbeya, ikiwa na lengo kuu la “Kuimarisha ufanisi na uzingatiaji wa ulipaji kodi kupitia mifumo ya kidijitali.”Akifungua mafunzo hayo, Meneja wa TRA Mkoa wa Mbeya, Musibu Shaban, aliwapongeza wadau wa kodi na wafanyabiashara wa mkoa huo kwa ushirikiano mkubwa wanaouonesha kwa Serikali, hali iliyowezesha Mkoa wa Mbeya kuendelea kuvuka malengo ya makusanyo ya kodi.Shaban aliwapongeza kwa namna ya pekee wafanyabiashara kwa kulipa kodi kwa hiari bila shuruti, akieleza kuwa hatua hiyo inaonesha uzalendo na uelewa mkubwa wa wananchi wa Mbeya kuhusu umuhimu wa kodi katika maendeleo ya Taifa.“Mmekuwa mkivuka malengo mara kwa mara na kupitia mafunzo haya yaliyofanyika leo yataendelea kwa pia kwa wiki ijayo ili kuhakikisha wadau wote wanaelewa kikamilifu mfumo huu mpya,” alisema Shaban.Akiendelea kutoa elimu, Meneja huyo alieleza kuwa Mfumo wa ukusanyaji wa Kodi za Ndani (IDRAS) ni mfumo jumuishi unaotarajiwa kuzinduliwa rasmi Februari 9, 2026, wenye lengo la kupanua wigo wa kodi na kuhakikisha usawa katika ukusanyaji wake.Alifafanua kuwa IDRAS unaunganisha huduma zote za usimamizi wa kodi kuanzia usajili wa walipa kodi, ulipaji wa kodi, ufuatiliaji hadi usimamizi wa taarifa zote za kodi kupitia jukwaa moja la kidijitali.“Kwa sasa mambo yamerahisishwa sana tofauti na zamani hakuna tena usumbufu wa kutembea ofisi mbalimbali mtu anaweza kujisajili mwenyewe akiwa popote alipo kupitia mfumo,” aliongeza Shaban.Alisisitiza kuwa mfumo huo mpya utaongeza ufanisi, kupunguza matumizi ya makaratasi na kuboresha huduma kwa walipa kodi, huku ukiongeza uwajibikaji na kurahisisha utunzaji wa kumbukumbu za kifedha.Aidha, alisema IDRAS utawezesha mifumo mingine ya Serikali kuunganishwa kwa urahisi zaidi, hatua itakayochochea uwazi na nidhamu ya ukusanyaji wa mapato ya ndani.Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Mowi Consulting, CPA Baraka Mori, alisema taasisi hiyo inajihusisha na kutoa huduma za ushauri wa kitaalamu katika masuala ya kodi na uhasibu, ikiwemo uratibu wa masuala ya kodi, usimamizi wa mashauri ya kodi ya TRA, uandishi wa mipango ya biashara, utunzaji wa vitabu vya kumbukumbu za kifedha (book keeping), pamoja na uwasilishaji wa marejesho ya VAT, PAYE, SDL, NSSF, WCF na maandalizi ya mishahara (payroll).Mori aliongeza kuwa Mowi Consulting imejidhatiti kutoa ushauri wa kitaalamu wa biashara katika maeneo ya uhasibu, kodi, usimamizi wa fedha, uongozi na uendeshaji wa biashara, ikiwa ni sehemu ya mchango wake katika kukuza uchumi na kuongeza uelewa wa masuala ya kodi kwa wafanyabiashara.
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254




Post a Comment