Na Mwandishi wetu, Misalaba Media
Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbawara, amefanya ziara ya kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa Bandari ya kisasa ya Mbamba Bay iliyopo Wilaya ya Nyasa, Mkoa wa Ruvuma. Katika ziara hiyo, Waziri ameonesha kuridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi huo ambao umefikia asilimia 47, huku akibainisha kuwa unatarajiwa kukamilika kabla ya tarehe 26 Agosti mwaka huu.
Profesa Mbawara amesema Serikali inatambua umuhimu mkubwa wa bandari hiyo kwa wananchi wa kanda ya Nyasa na maeneo ya jirani, akisisitiza kuwa wananchi wamekuwa wakiisubiri kwa muda mrefu. Amesema Serikali itaendelea kufanya kila linalowezekana kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyostahili ili kuleta tija iliyokusudiwa.
Ameongeza kuwa ujenzi wa bandari hiyo umezingatia mabadiliko ya tabia ya nchi kwa kipindi cha miaka 50 ijayo, ili kuhimili mabadiliko ya viwango vya maji ikiwemo kupanda na kushuka. Hatua hiyo inalenga kuhakikisha bandari inafanya kazi kwa ufanisi na usalama kwa muda mrefu bila kuathiriwa na athari za mazingira.
Waziri Mbawara pia ametoa wito kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) pamoja na mkandarasi wa mradi huo kuhakikisha wanasimamia kikamilifu ratiba ya ujenzi ili kukamilisha kazi kwa wakati uliopangwa, akisisitiza umuhimu wa uwajibikaji na usimamizi madhubuti wa mradi.
Akijibu ombi la Mbunge wa Jimbo hilo, Mhe. John Nchimbi, kuhusu fidia kwa wananchi waliopisha mradi, Waziri amesema Serikali inawapenda Watanzania na itaendelea kuhakikisha haki inatendeka. Ameeleza kuwa wananchi wa eneo hilo tayari wamefanyiwa tathmini, na wataalamu wanatarajiwa kufika kufanya uhakiki wa mwisho kabla ya malipo ya fidia kufanyika kwa mujibu wa sheria.
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254






Post a Comment