Baadhi ya vijana nchini wameishauri Serikali kuendelea kuweka kipaumbele katika kutatua changamoto zinazolikabili kundi hilo, huku wakisisitiza kuwa njia ya mazungumzo na utii wa sheria ndiyo msingi wa kudumisha amani ambayo Tanzania imekuwa kimbilio kwa miaka mingi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, vijana hao wameeleza kuwa taifa linapaswa kujifunza kutoka kwa waasisi na watangulizi ambao walichagua kukaa meza moja na kuzungumza badala ya kuchochea migogoro ambayo ingeweza kulisambaratisha taifa.
Umuhimu wa Mazungumzo na Kujifunza kutoka kwa Watangulizi
Mmoja wa vijana hao ametoa rai kwa kizazi cha sasa kuacha mawazo ya machafuko, akitolea mfano nchi jirani ambazo zimeingia kwenye migogoro ya muda mrefu.
“Wazazi wetu kama mambo yaliyowachosha wangeamua kuleta ugomvi tungekuwa wapi? Waliketi wakazungumza. Na sisi pia tupate nafasi hiyo tuketi tuzungumze ili tusaidie kusonga mbele na kuachana na uwezekano wa machafuko. Tangu tumezaliwa tunasikia wenzetu kama Wakongo wanapigana, na hili si jambo zuri. Tanzania ndio kimbilio la wengi, tukipigana sisi inakuwaje?” alihoji mmoja wa vijana hao.
Wajibu wa Serikali na Haki za Vijana
Kwa upande wake, Veronica John, mkazi wa Mkoa wa Tanga, amesisitiza kuwa ili amani idumu, Serikali inapaswa kujenga utaratibu madhubuti wa kuwasikiliza vijana na kuwapa nafasi ya kueleza kero zao. Alibainisha kuwa kusikilizwa kwa kundi hilo kutasaidia kuzuia manung’uniko na kuimarisha mshikamano wa kitaifa.
Naye Frank Gelvas, kijana kutoka mkoani Kagera, amekumbusha kuwa mbali na Serikali kutoa fursa za ajira, vijana wana wajibu wa kutii mamlaka na viongozi waliopo madarakani. Amesema kudai haki siyo sababu ya kufanya vurugu, bali ni fursa ya kutumia njia za kistaarabu.
Fursa za Kiuchumi na Kazi
Mbali na masuala ya kisiasa na kijamii, vijana wamehimizwa kutumia rasilimali ambazo Mungu amelijalia taifa la Tanzania. Wamehimizwa kuchapa kazi kwa kutumia ardhi yenye rutuba, maziwa kwa ajili ya uvuvi, na bahari ili kujikwamua kiuchumi.
“Nchi yetu ina kila kitu; ina ardhi, maziwa na bahari. Vijana tuchape kazi na tujishughulishe na uchumi kwani Mungu ametujalia fursa nyingi,” aliongeza kijana mwingine katika mfululizo wa maoni hayo.
Wito huo wa vijana unakuja wakati ambapo Serikali inaendelea kuimarisha mifuko ya kutoa mikopo kwa vijana, wanawake na wenye ulemavu, huku ikiimarisha mazingira ya uwekezaji ili kutengeneza fursa nyingi zaidi za ajira nchini.
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

Post a Comment