Wafanyabiashara wadogo na viongozi wa Shirikisho la Umoja wa Machinga (SHIUMA) mkoani Pwani wamesisitiza kuwa amani ndiyo msingi mkuu wa maendeleo ya kiuchumi, huku wakitoa wito kwa wananchi kudumisha utulivu ili kulinda haki zao za kufanya kazi na kutekeleza wajibu wao wa kujenga taifa.
Akizungumza hivi karibuni, Mwenyekiti wa SHIUMA Mkoa wa Pwani, Filemon Maliga, amesema kuwa amani ndio rasilimali ya kwanza kwa mfanyabiashara yeyote kabla hata ya fedha.
“Mtaji wa sisi wamachinga ni amani. Hata wawekezaji wanawekeza sehemu yenye amani. Pia tunahitaji utulivu ili wateja waweze kuja kununua vitu tunavyouza. Tuendeleze na mshikamano tulio nao kwa ajili ya maendeleo yetu na taifa kwa ujumla,” alisema Maliga.
Kauli hiyo imechagizwa na wafanyabiashara wa soko la Michonjo Uyaoni lililopo Kibaha, ambao wamebainisha kuwa bila utulivu, mzunguko wa fedha na maisha ya kila siku yatasimama, jambo litakalowaathiri zaidi watu wa hali ya chini.
Amani na Utekelezaji wa Majukumu ya Kila Siku
Kwa upande wake, Joyce Mramba, mfanyabiashara katika soko la Michonjo, ameeleza kuwa amani inampa mfanyabiashara uhuru wa kutafuta riziki. Alibainisha kuwa biashara nyingi zinategemea kutoka nje na kukutana na watu, jambo ambalo haliwezekani pasipo utulivu.
“Tunaendelea kuipigania amani ya nchi yetu kwani amani ikikosekana inasababisha tushindwe kufanya shughuli zetu. Tunaiombea nchi yetu ili iwe na utulivu ili tufanye shughuli zetu za kila siku na tudumishe mshikamano wetu,” alisema Joyce.
Changamoto ya Mikopo na Wito kwa Vijana Naye
Mwenyekiti wa Soko la Michonjo, Iddi Bundala, amehusisha amani na uwezo wa wafanyabiashara kulipa madeni yao. Ameeleza kuwa biashara nyingi kwa sasa zinaendeshwa kwa mikopo, hivyo vurugu zozote zinaweza kusababisha hasara kubwa na kushindwa kurejesha fedha hizo.
“Tunahitaji amani ili tufanye biashara zetu kwani amani ikivunjika tutashindwa kufanya biashara. Mitaji tumekopa, hivyo tusipofanya biashara tutashindwa kufanya marejesho ya mikopo,” alisisitiza Bundala.
Aidha, alitoa wito maalum kwa vijana nchini kuepuka kujiunga na makundi yanayoweza kuchochea uvunjifu wa amani, akisisitiza kuwa jukumu la kujenga nchi ni la kila mmoja.
Habari hii inakuja wakati ambapo wadau wa maendeleo wameendelea kusisitiza kuwa amani ya Tanzania ndiyo kivutio kikubwa cha uwekezaji na chachu ya ustawi wa wananchi wake, hasa katika kipindi hiki ambacho taifa linajikita katika kukuza uchumi wa viwanda na biashara ndogondogo.
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

Post a Comment