" UVCCM KAGERA WASHEREKEA SIKU YA KUZALIWA YA RAIS SAMIA KWA KUPANDA MITI 2,000 OMUMWANI SECONDARI

UVCCM KAGERA WASHEREKEA SIKU YA KUZALIWA YA RAIS SAMIA KWA KUPANDA MITI 2,000 OMUMWANI SECONDARI



BUKOBA KAGERA.

Umoja wa Vijana chama cha Mapinduzi (UVCCM)mkoani Kagera, ikiongozwa na Mwenyekiti wake Faris Buruhan, imeadhimisha siku ya kuzaliwa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kupanda miti 2,000 katika Shule ya Sekondari Omunwani, iliyopo wilayani Bukoba.

‎Akizungumza mara baada ya zoezi hilo, Faris amesema kuwa lengo la tukio hilo ni kuunga mkono jitihada za Rais Samia katika kulinda na kutunza mazingira, akisisitiza kuwa upandaji wa miti ni sehemu muhimu ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Ameongeza kuwa jumuiya hiyo imeamua kuonyesha uzalendo wa vitendo kwa kushiriki katika shughuli zenye manufaa kwa jamii na taifa kwa ujumla.

‎Faris amewahimiza wananchi wa Kagera na Watanzania kwa ujumla kupanda miti katika maeneo yao na kuitunza ipasavyo, akieleza kuwa utunzaji wa mazingira ni jukumu la kila mmoja. Amesema hatua hiyo itasaidia kulinda vyanzo vya maji, kuboresha hali ya hewa na kuhakikisha maisha endelevu kwa vizazi vijavyo.

‎Kwa upande wao, baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari Omunwani,Brandina Conrad,Diana Wilbroad na Tausi Kassim wameishukuru Jumuiya ya Vijana wa Kagera kwa kutoa miche 2,000 ya miti kwa ajili ya kuboresha mazingira ya shule hiyo. Wamesema upandaji wa miti una faida nyingi ikiwemo kuboresha mazingira ya kujifunzia, kivuli na hewa safi, huku wakiahidi kuitunza miti hiyo hadi ikue.

‎Naye Mhifadhi Misitu wa Wilaya ya Bukoba Anatory Lagweni amewahimiza wananchi kupanda miti ya aina mbalimbali katika makazi yao na maeneo ya wazi, akisisitiza umuhimu wa kushiriki kikamilifu katika juhudi za kuhifadhi mazingira na misitu kwa maendeleo ya sasa na baadaye.

‎Kwingineko, Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Faris Buruhan, ameomba Serikali kusaidia ujenzi wa uzio katika Shule ya Sekondari Omunwani ili kuimarisha usalama wa wanafunzi na kulinda miundombinu ya shule hiyo.

‎Ikumbukwe kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan huadhimisha siku yake ya kuzaliwa kila mwaka tarehe 27 Januari, huku kaulimbiu ya “Uzalendo ni Kutunza Mazingira, Shiriki Kupanda Miti” ikiendelea kuhamasisha jamii kushiriki katika uhifadhi wa mazingira.










Post a Comment

Previous Post Next Post