Na Fabius Clavery, Misalaba Media-Kagera.
Wananchi mbalimbali mkoani Kagera wameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutekeleza miradi ya ujenzi wa madaraja katika maeneo yaliyokuwa korofi, hali iliyokuwa ikisababisha kukatika kwa mawasiliano ya barabara hususan wakati wa msimu wa mvua.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wananchi wamesema kabla ya ujenzi wa madaraja hayo walikuwa wakikumbana na changamoto kubwa za usafiri, ikiwemo kuchelewa kufika maeneo ya jirani pamoja na kulazimika kuzunguka umbali mrefu ili kufanikisha shughuli zao za kijamii na kiuchumi.
Baadhi ya wakazi wa Kata ya Kishogo, Wilaya ya Bukoba, Bwana Kelvin Paul,Shabani Ahmad Baguma na Musharraf Mudy, amesema ujenzi wa Daraja la Kyanyabasa utaleta mabadiliko makubwa kwa wakazi wa kata hiyo pamoja na kata jirani, hasa katika kurahisisha safari na usafirishaji wa mazao na malighafi mbalimbali kwenda sokoni.
Wameeleza kuwa kabla ya kuanza kwa ujenzi wa daraja hilo, wananchi walilazimika kutumia kivuko ambacho kilikuwa hatarishi, hasa nyakati za mvua ambapo maji yalikuwa yakiongezeka na kukifanya kivuko hicho kushindwa kutoa huduma kwa uhakika.
Kwa upande wake, Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Kagera, Mhandisi Samwel Joel Mwambungu, amewataka wananchi watakaonufaika na miradi hiyo kuhakikisha wanayatunza madaraja hayo na kuepuka kuyaaribu, akisisitiza kuwa madaraja hayo yamejengwa ili kuondoa adha kubwa ya usafiri waliyoipitia kwa muda mrefu.
Naye Mhandisi John Andrew, msimamizi wa mradi huo kutoka kampuni ya Gemen Engineering Constructors, amesema licha ya changamoto mbalimbali zilizojitokeza ikiwemo kina kirefu cha maji, mkandarasi anaendelea na kazi kwa kasi na mradi unatarajiwa kukamilika kwa wakati uliopangwa.
Daraja la Kyanyabasa lenye urefu wa mita 105 linajengwa na mkandarasi mzawa Gemen Engineering Constructors, na ni miongoni mwa madaraja matano yanayoendelea kujengwa mkoani Kagera yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 45. Miradi hiyo inatekelezwa chini ya Mradi wa Ujenzi wa Madaraja ya Dharura (SEQ), kufuatia mvua kubwa za El Niño zilizonyesha mapema mwaka 2024 na kusababisha uharibifu wa miundombinu ya barabara katika mikoa mbalimbali nchini.
Madaraja mengine yanayotekelezwa chini ya mradi wa SEQ mkoani Kagera ni pamoja na Daraja la Kanoni linalojengwa na Abemulo Contractors, Daraja la Kamishango lililopo Wilaya ya Muleba linalotekelezwa na DRK Contractors, Daraja la Kyetema linalotekelezwa na Gemen Engineering Constructors, pamoja na Daraja la Karebe linalojengwa na Milembe Constructors Ltd.




Post a Comment