
Na. Meleka Kulwa- Dodoma.
Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, amesema kuwa utoaji wa huduma bora za afya ni msingi wa heshima ya maisha ya binadamu na haupaswi kuathiriwa na uzembe, ucheleweshaji wa maamuzi au udhaifu wa mifumo ya uendeshaji wa hospitali.
Mhe. Mchengerwa ameyasema hayo Januari 14, 2026, wakati wa kikao kazi kilichofanyika Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) jijini Dodoma, kilichowakutanisha Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Afya pamoja na watumishi wa sekta ya afya wa Mkoa wa Dodoma.
Amesema kuwa wananchi wanaofika hospitalini wanapaswa kupata huduma bora bila visingizio, akibainisha kuwa imani ya mwananchi kwa mfumo wa afya hujengwa na kuvunjwa kupitia namna huduma inavyotolewa. Amebainiaha kuwa katika sekta ya afya hakuna nafasi ya kusema huduma imetolewa kadri ya uwezo bila kuzingatia matokeo kwa mgonjwa.
Amebainisha kuwa utoaji wa huduma bora unapaswa kutegemea mifumo imara inayofanya kazi muda wote, badala ya utegemezi wa mtu mmoja au uzoefu binafsi wa mhudumu. Amesema kuwa ubora wa huduma haupaswi kubadilika kulingana na nani yupo kazini bali uwe sehemu ya utamaduni wa taasisi za afya.
Aidha, Waziri mchengerwa amesisitiza umuhimu wa hospitali kuzingatia taratibu zilizoandikwa na zinazofuatwa, pamoja na kupima matokeo ya huduma zinazotolewa ili kubaini mapungufu na kuyarekebisha kwa wakati. Amebainisha kuwa kujifunza kutokana na makosa na kulinda usalama wa wagonjwa na wahudumu ni sehemu muhimu ya utoaji wa huduma bora.
Mhe. Mchengerwa amesema kuwa kutoa huduma kwa wananchi si hisani bali ni haki, kwa kuwa wananchi wanalipa kodi na kuchangia maendeleo ya sekta ya afya. Ameeleza kuwa serikali na watumishi wa afya wana wajibu wa kuhakikisha huduma zinazotolewa zinakidhi hadhi ya maisha ya binadamu.
Katika maelekezo yake, amesema kuwa maamuzi ya haraka na sahihi ni sehemu ya utoaji wa huduma bora, akibainisha kuwa mgonjwa hana muda wa kusubiri urasimu wa barua nyingi au vikao visivyo na maamuzi. Amesema kuwa ucheleweshaji wa maamuzi unaweza kusababisha gharama kubwa ikiwemo kupoteza maisha ya wagonjwa.
Ameongeza kuwa viongozi wa sekta ya afya wanapaswa kutumia mamlaka waliyopewa kutatua matatizo yanapojitokeza badala ya kusubiri maagizo kwa kila hatua, akisisitiza kuwa uamuzi ni hatua ya kwanza ya matibabu.
Awali, akizungumza katika kikao hicho, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Profesa Abel Makubi, amesema kuwa hospitali hiyo imepiga hatua kubwa katika utoaji wa huduma za kibingwa na kibobezi tangu kuanzishwa kwake.
Amesema kuwa katika kipindi cha miaka kumi, hospitali imeanzisha huduma za kibingwa 20 na 18 zikiwa za kibobezi (ubingwa wa Juu) ,huku asilimia 60 ya huduma hizo zikianzishwa ndani ya miaka minne ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Aidha amebainisha kuwa baadhi ya huduma hizo ni pamoja na upandikizaji wa figo, upandikizaji wa uloto, upasuaji wa moyo kwa watoto na watu wazima, uchunguzi na uzibaji wa mishipa ya moyo, radiolojia ya kimataifa, uvunjaji wa mawe kwa mawimbi, matibabu ya homoni, magonjwa ya mfumo wa chakula, upasuaji wa ubongo na uti wa mgongo, upasuaji wa mifupa ikiwemo nyonga na magoti, pamoja na huduma za utalii wa matibabu na uchunguzi wa afya ya kina.
Prof. Makubi amesema kuwa hadi Januari 13, 2026, Hospitali ya Benjamin Mkapa ikiwa na watumishi 1,073, wakiwemo madaktari bingwa wa juu zaidi ya 100, imefanikiwa kufanya upandikizaji wa figo kwa wagonjwa 54 kwa gharama ya shilingi bilioni 6, ikilinganishwa na zaidi ya shilingi bilioni 7 ambazo zingetumika kama wagonjwa hao wangefanyiwa matibabu nje ya nchi.
Amesema mafanikio hayo ni matokeo ya uwekezaji mkubwa wa Serikali katika sekta ya afya na dhamira ya dhati ya kuboresha huduma za kibingwa kwa wananchi ndani ya nchi.

🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254
Post a Comment